Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema, inaunga mkono mpango ulioandaliwa na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST), katika utowaji wa mafunzo ya huduma za ndege katika Viwanja vya Ndege.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw.Khamis Abdalla Said, amesema hayo alipokuwa katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya utowaji wa mafunzo hayo kwa Taasisi ya Karume na Wataalamu wa huduma za ndege katika viwanja vya ndege, hafla ilifanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Dkt. Idrissa Muslim Hijja Bweni Zanzibar.
Amesema, hatua hiyo inakwenda sambamba na dhamira ya Serikali juu ya kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini.
Amesema, kuwepo kwa mafunzo hayo itachochea kupatikana Wafanyakazi wa kutosha wenye utaalamu wa kutoa huduma kwa kiwango kinachohitajika.
Aidha, Bw.Said amefahamisha kuwa, Vijana wengi wanamaliza elimu zao na kubakia mitaani kufanya mambo yasiostahiki hivyo, kuwepo kwa mafunzo hayo itakuwa chachu ya kutimiza ndoto zao na kuipunguzia mzigo Serikali.