Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Nd. Khamis Abdullah Said amesema Kufanyika kwa Maonesho ya Wiki ya Elimu ya Juu Kisiwani Pemba Kuna lengo la kuwasogezea Wanafunzi huduma kwa ukaribu ili waweze kufanya maamuzi sahihi ya Kimasomo.

Ameyasema hayo wakati akifunga Wiki ya Maonesho ya Elimu ya Juu huko katika Uwanja wa Gombani Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Amewataka Wanafunzi  pamoja na Wazazi kuyafanyia kazi maelekezo waliyoyapata kutoka  Vyuo mbali mbali  kabla ya kutoa maamuzi yao.

Akizungumzia jitihada za Serikali katika kuwapatia Wanafunzi fursa za kujiendeleza kielimu Katibu Mkuu amesema Serikali inafanya utaratibu wa kubadilisha sheria ya Bodi ya Mikopo Zanzibar ili huduma zao ziweze kupatikana hadi ngazi ya Stashahada.

Akifafanua zaidi Nd. Said amesema  Serekali zote mbili ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania na Serekali ya Mapinduzi Zanzibar kwasasa zinatoa huduma ya mikopo ili kujiendeleza kuanzia Ngazi ya Shahada.

Akitoa pongezi kwa Vyuo ambavyo vimeshiriki amesema Maonesho hayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuongezeka upkwa udahili kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikiwemo na vya Kati.

Nae Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mwalimu Moh'd Nassor Salim amesema Wizara inafanya  maboresho ili Maonesho ya ya mwaka 2024 yaweze Kufanyika kwa  Bora zaidi. 

Amesema Maonesho hayo yanasaidia kwa kiasi kikubwa  kuondosha Changamoto kwa vijana kuweza kuchagua fani mbali mbali kulingana na Ufaulu wao.

Kwa Upande wake Meneja wa Bank ya  NMB ambayo imedhamino Maonesho hayo Nd. Hamad Mussa Msafiri amesema Bank hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu katika kuendeleza gurudumu la Elimu Nchini.

Aidha amesema NMB imeanzisha Mfuko Maalumu unaojulikana kwa Lina la "Nuru Yangu" ambao unawasaidia Wanafunzi Wenye mazingira magumu.

Awali Kaimu Mratibu Kitengo Cha Uratibu wa Elimu ya Juu Mr. Hamad Mkubwa Hamad amesema Maonesho ya mwaka huu yamepokea jumla ya Wanafunzi 3000 ukilinganisha na 1600 idadi ya mwaka Jana.