Mkurugenzi Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima Bi Mashavu Abdallah Fakihi amesema Idara itaendelea kufanya jitihada za kuwarejesha katika mfumo rasmi wa Elimu waliotoroka na Waliokosa huduma hiyo.

Bi Mashavu ameyasema hayo wakati Akizungumza na Wazazi pamoja na Wanafunzi wa Elimu Mbadala kwa nyakati tofauti katika Hafla ya Ugawaji wa Vifaa kwa Wanafunzi huko katika Skuli ya Kengeja Wilaya ya Mkoani  na Skuli ya Uwandani Wilaya ya Chake Chake ikiwa nishamrashamta za kuelekea kilele Cha Maadhimisho ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima.

Amesema Idara imeshapiga hatua kwa asilimia 90 kupitia Mradi unaofadhiliwa kwa Mashirikiano ya pamoja kati ya UNICEF, Qatar na SMZ wenye Lengo la kuwarejesha Wanafunzi waliotoroka Skuli.

Aidha Bi Mashavu amesema  ugawaji wa vifaa utawasaidia Wanafunzi hao kuweza kupata hamasa na hamu yakuendelea na masomo na kujikomboa katika maisha yao ya baadae.

Aidha Bimashavu amewataka Walimu kutotumia lugha za kuwavunja moyo Wanafunzi hao na badala yake wajenge urafiki ili waweze kutambua Changamoto zao kwa urahisi.

Kwa Upande wake Mratibu Idara ya Utumishi na Uendeshaji Mwalimu Harithi Bakari Waziri Akizungumza kwa Niaba ya Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu ameishukuru Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima kwa kuwapa motisha Wanafunzi hao.

Amesema kupatiwa vifaa kwa Wanafunzi hao kutaongeza Ari na moyo wa kujisomea sambamba na kuibua utayari wa kujiunga na Masomo kwa Wanafunzi wengine ambao bado hawajarejea Masomoni.

Nae Mratibu Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima Nd. Salim Kuza Sheikhan amesema Idara imefanikiwa kusaidia kuandikishwa Skuli Wanafunzi takriban 11,000 ambao walishapindukia umri sahihi Wakuandikishwa Skuli.

Aidha amesema mbali na kuwarejesha Skuli Wanafunzi hao Idara inaendelea kufanya jitihada za kufungua madarasa ya kisomo Cha Watu Wazima ili kuondosha kabisa tatizo la Watu Kutokujua kusoma, kuandika na kuhesabu.