THE Revolutionary Government of Zanzibar

Ministry of Education and Vocational Training

Education History

Kabla ya kuingia wakoloni katika nchi yetu, Zanzibar ilikuwa na mfumo wake wa elimu. Mfumo wa Elimu wa jadi ambao ulitilia mkazo katika kuwawezesha vijana kujitegemea na kuwafanya vijana kuuelewa, kuuthamini na kuuenzi utamaduni wao wa asili. Elimu ya jadi ilijumuisha pamoja na mambo mengi mengine, namna ya kuishi katika jamii, tiba za asili, kutengeneza vifaa mbali mbali vya kuzalisha mali kama zana za kilimo, uvuvi, ufugaji na kadhalika. Kwa ujumla mfumo wa elimu ya jadi ulikuwa umekomaa na wakati wakoloni wanaingia katika nchi yetu waliikuta jamii ikiwa tayari na mfumo wake wa maisha.

Wakoloni walipokuja Zanzibar, jambo la mwanzo walilofanya ni kujaribu kubadilisha mfumo wa maisha ambao ungekidhi mahitaji yao. Wakoloni waliamua kuanzisha mfumo wa elimu wa kimagharibi kwa lengo la kuwapata watu wachache watakaoweza kuutumikia utawala wa kikoloni na kisultani uliokuwepo wakati huo. Kwa hivyo, elimu ilitolewa kwa misingi ya kitabaka na makabila, kulingana na hadhi ya tabaka au kabila hilo mbele ya utawala wa kikoloni na kisultani.

Historia ya elimu ya magharibi hapa Zanzibar ilianzia mwaka 1890 wakati skuli ya mwanzo iliyojulikana kwa jina la Sir Euan Smith Madressa ilipoanzishwa na jamii ya Wahindi kwa ajili ya kuwapatia elimu watoto wao. Katika mwaka 1907, utawala wa kifalme ulianzisha skuli kwa ajili ya watoto wa aila yao tu. Mwaka 1920, utawala wa Kiingereza ulianza kutoa elimu kwa watu wengi kwa misingi ya kibaguzi.

Watu wenye asili ya Asia na ya Kiarabu walipangiwa kupatiwa elimu ya msingi na sekondari kwa muda wa miaka 12. Watu wenye asili ya Kiafrika ambao ndio wengi walipangiwa miaka minne tu ya elimu ya msingi.

Kutokana na ubaguzi waliokuwa wakifanyiwa Waafrika wanyonge walio wengi katika utoaji wa elimu, na kutokana na umuhimu wa elimu katika kuleta maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa jumla, Chama cha ASP kilipokuwa katika harakati za kupigania uhuru kiliweka bayana katika manifesto yake kwamba pindipo kikishika hatamu ya uongozi wa nchi, Serikali itayoongozwa na ASP itatoa elimu bila ya malipo na bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Baada ya kushindikana mbinu zote za kudai uhuru kwa njia ya amani, wananchi wazalendo wa Zanzibar chini ya uongozi wa Chama cha ASP na Rais wa ASP, Marehemu Mzee Abeid Amani karume, walifanya Mapinduzi tarehe 12 Januari 1964, ili kuung’oa utawala wa kikoloni na kisultani. Mara tu baada ya kushika hatamu, Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, siku ya tarehe 23 Septemba, 1964, alitoa tamko kwamba elimu Zanzibar itatolewa bila ya malipo na bila ya ubaguzi wa aina yo yote.

Tangu wakati huo, Serikali za awamu zote chini ya uongozi wa ASP wakati huo na sasa Chama cha Mapinduzi (CCM) zimekuwa zikitekeleza kwa vitendo sera ya elimu bila ya malipo na mafanikio makubwa na ya kupigiwa mfano yamepatikana.

Baada ya Mapinduzi Matukufu, Serikali ilirithi mfumo wa elimu wa kikoloni wa 8 – 4 – 2, yaani miaka minane ya elimu ya msingi, miaka minne ya sekondari ya kawaida na miwili ya sekondari ya juu. Baada ya kipindi cha miaka 40 ya mapinduzi matukufu, mfumo wa elimu wa elimu ulibadilika na kuwa na muundo wa 3 – 7 – 3 – 2 – 2, yaani miaka mitatu ya elimu ya maandalizi, miaka saba ya elimu ya msingi, miaka mitatu ya sekondari ya awali, miaka miwili ya sekondari ya kawaida na miaka miwili ya sekondari ya juu. Miaka saba ya elimu ya msingi na mitatu ya sekondari ya awali hufanya elimu ya lazima, ambayo ni haki ya kila mtoto wa nchi hii.

Huduma zetu ni pamoja na :-

  • Kuratibu na kutayarisha Mitaaala ya Elimu
  • Kutoa miongozo ya kufundishia na kujifunzia
  • Kupanga na kutoa viwango vya ufaulu wa Elimu
  • Kusimamia maendeleo ya Elimu
  • Kusimamia, kufuatilia na kutathmini mipango ya maendeleo ya Elimu
  • Kutoa miongozo ya Elimu maalumu
  • Kuandaa Sera ya Elimu
  • Kutoa miongozo ya uanzishaji wa Skuli binafsi na jamii
  • Kusajili Skuli za binafsi, Skuli za jamii na vituo vya kujiendeleza
  • Kushughulikia maombi na kutoa leseni za walimu za kufundishia
  • Kutoa miongozo kuhusu uhamisho wa wanafunzi
  • Kuandaa Mitihani ya Taifa kwa ngazi ya msingi, sekondari na vyuo vya ualimu
  • Kusimamia na kuweka uwiano baina ya walimu na wanafunzi
  • Kutoa miongozo ya uongozi na utawala katika skuli,vituo na vyuo vya ualimu
  • Kushughulikia madai ya maslahi ya wafanyakazi
  • Kuwapangia kazi watumishi wa Wizara kwa mujibu wa mahitaji
  • Kuratibu huduma za TEHAMA katika Elimu
  • Kutoa na kusimamia mafunzo ya watumishi
  • Kutoa na kusimamia mafunzo ya ualimu
  • Kusimamia ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia
  • Kuratibu ajira, kuthibitisha na kupandisha cheo watumishi
  • Kukamilisha majengo ya skuli yaliyoanzishwa na wananchi
  • Kuratibu na Kusimamia shughuli za Michezo na sanaa.