THE Revolutionary Government of Zanzibar

Ministry of Education and Vocational Training

WAZIRI LELA AKABIDHI ENEO LA UJENZI WA SKULI YA GHOROFA NNE SHAMIANI, ATAKA UBORA NA UKAMILISHWAJI KWA WAKATI.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mheshimiwa Lela Muhamed Mussa, amekabidhi rasmi eneo la ujenzi wa skuli mpya ya ghorofa nne katika eneo la Shamiani, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu ya elimu na kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Akizindua utekelezaji wa mradi huo, Mhe. Lela amewataka wananchi wa Shamiani na maeneo ya jirani kushirikiana kikamilifu na mkandarasi ili kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa ufanisi bila vikwazo.

Aidha, amemtaka mkandarasi kuzingatia masharti yote ya mkataba, kuhakikisha ubora wa kazi na kukamilisha mradi ndani ya muda uliopangwa.

Katika kuhakikisha jamii inanufaika moja kwa moja na mradi huo, Waziri ameelekeza ajira za vibarua kutolewa kwa vijana wanaoishi katika eneo la Shamiani na maeneo ya jirani.

Mhe. Lela amesema skuli hiyo itakapokamilika itakuwa na samani pamoja na vifaa vya kisasa vitakavyowezesha mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji. Kutokana na uwekezaji huo mkubwa wa Serikali, amewataka walimu kuongeza juhudi katika ufundishaji ili matokeo ya taaluma yaakisi kiwango cha uwekezaji huo.

Akiwasilisha taarifa ya kiufundi ya mradi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ndg. Amos John Henock, amesema jengo hilo la ghorofa nne litakuwa na jumla ya madarasa 51 pamoja na maabara za kisasa, vyumba vya walimu na miundombinu mingine muhimu ya kijamii na kiutawala.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake, Mheshimiwa Abdulwahab Said Abubakar, ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuleta mradi huo mkubwa ambao utapanua fursa za elimu kwa watoto wa Shamiani na maeneo jirani.

Aidha, ameiomba Serikali kuipatia skuli hiyo huduma ya usafiri wa wanafunzi (dahalia) ili kurahisisha usafiri kwa wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali.

Mradi wa ujenzi wa skuli hiyo unatekelezwa na Kampuni ya Mwinyi Building Contractor, huku usimamizi wa kitaalamu ukifanywa na Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA).