
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Sekondari, Bi Asya Iddi Issa, amewataka walimu na wanafunzi kudumisha usafi wa mwili na mazingira ya skuli kwa ujumla.
Akizungumza leo tarehe 28 Julai 2026, wakati wa hafla ya makabidhiano ya miundombinu ya usafi iliyoboreshwa kwa skuli za sekondari kati ya Wizara hiyo na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA), iliyofanyika katika Skuli ya Sekondari Chumbuni, Bi Asya amesema walimu wanapaswa kutumia mafunzo waliyopewa kuwaongoza wanafunzi juu ya umuhimu wa usafi.
Ameeleza kuwa usafi ni msingi muhimu wa afya na mazingira bora ya kujifunzia, hivyo ni wajibu wa walimu na wanafunzi kuhakikisha wanatunza mazingira ya skuli wakati wote.
Aidha, ametoa shukrani kwa Shirika la KOICA kwa mchango wake mkubwa wa kutoa elimu ya usafi, kujenga kisima pamoja na kuboresha huduma ya maji, hatua ambayo imeisaidia skuli kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji. Ameahidi kuwa Wizara itaendelea kusimamia na kutunza mradi huo ili uweze kuleta manufaa endelevu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la KOICA, Bw. Sikhyon Kim, amesema kukamilika kwa mradi huo ni mwanzo wa hatua nyingine za maendeleo. Amewahimiza walimu kuhakikisha wanaweka mazingira bora na kusimamia ipasavyo miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kuleta tija kwa wanafunzi.
Mradi huo wa kuimarisha huduma ya maji na kudumisha usafi umetekelezwa katika skuli tano za sekondari, zikiwemo Skuli ya Sekondari Chumbuni, Fukuchani, Machui na Chaani.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano WEMA.