
Naibu katibu mkuu taaluma wa wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar Dkt Mwanakhamis Adam Ameir amesema ni vyema kushirikiana katika kuwasaidia vijana walioshindwa kujiendeleza na masomo yao ili kuwaendeleza kimaisha na kulisaidia taifa.
Ameeleza hayo leo tarehe 23 Juni 2026 katika mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu wa ZEPOSA na EPOSA huko katika ukumbi wa mikutano kituo cha elimu mbadala, Rahaleo Mkoa wa Mjini Magharibi – Unguja.
Dkt Mwanakhamis amefahamisha kuwa vijana hao kuna mambo mbali mbali yaliyowapelekea kukosa fursa ya kujiendeleza kielimu hivyo kila mmoja anawajibu wa kuwasaidi ili kuziba pengo walilolikosa na kujenga taifa bora la baadae.
Aidha amewasisitiza walimu watakaopatiwa mafunzo hayo kuelewa vizuri wanachofundishwa na kujielimisha zaidi ili kuweza kuwasaidia vijana hao kutimiza malengo yao.
Kwa upande wake Ndugu Frank Sabuwanka afisa kutoka wizara ya elimu, sayansi na teknolojia amesema program hiyo imeanzishwa ili kuonesha dhamira ya serikali katika kutoa fursa ya elimu kwa vijana wake, na kuwaweshesha hata wale ambao walishindwa kujiendeleza kupata fursa ya kujifunza kusoma kwa kutumia mifumo ya TEHAMA, kuandika, kuhesabu na ujasiriamali.
Nae mkurugenzi Idara ya elimu mbadala na watu wazima Ndugu Mashavu Ahmada Fakih amesema program ya ENUMA itakuwa mkombozi kwa vijana wasiojua kusoma na kuandika kujifunza kwa urahisi na ufasaha na kwa upande wa vituo vya elimu mbadala wamekuwa kukiwajengea uwezo vijana hao katika fani mbali mbali.
Imetolewa na Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano – (WEMA).