
Safari ya kuimarisha michezo skulini Zanzibar imepata msukumo mpya baada ya Idara ya Michezo na Utamaduni ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuendelea kusambaza vifaa vya michezo kwa skuli zilizopo katika mikoa yote ya Unguja na Pemba, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa wanafunzi katika michezo na kuendeleza vipaji vyao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo kwa Maafisa Elimu wa Mikoa ya Unguja, Mkurugenzi wa Idara ya Michezo na Utamaduni, Bi. Hafsa Aboud Talib, amewataka viongozi wa elimu kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kusimamia na kuendeleza michezo katika skuli zilizopo ndani ya wilaya na mikoa yao.
Amesema Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuimarisha sekta ya michezo katika elimu, hivyo ni wajibu wa wadau wote kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo yanayotarajiwa. Amesisitiza umuhimu wa Maafisa Elimu kushirikiana na Walimu Wakuu ili kutoa mazingira bora yatakayowezesha kuibua na kukuza vipaji vya wanafunzi kupitia michezo.
“Vifaa tunavyovitoa vitumike kwa wanafunzi wetu na visimamiwe ipasavyo ili viwe chachu ya maendeleo ya michezo katika skuli. Pia tumetoa mafunzo kwa walimu wa michezo na utamaduni kwa lengo la kuhakikisha michezo yote iliyopo katika Mwongozo Na. 4 wa Michezo inatekelezwa kwa ufanisi,” amesema Bi. Hafsa.
Ameongeza kuwa uwezo mkubwa unaooneshwa na wanafunzi katika mashindano mbalimbali ya kitaifa ni ushahidi kuwa uwekezaji unaofanywa katika michezo unaendelea kuzaa matunda, jambo linaloifanya Zanzibar kuendelea kufanya vizuri kila inaposhiriki mashindano hayo.
Vifaa vilivyokabidhiwa vinajumuisha viatu vya riadha, mpira wa miguu na mpira wa kikapu, shin guards, glovu za makipa, mipira ya michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mpira wa wavu na mpira wa mikono. Vifaa vingine ni vya michezo ya riadha kama matufe, mikuki, visahani na filimbi, pamoja na magoli na nyavu za michezo mbalimbali.
Hatua hiyo inaendelea kudhihirisha dhamira ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya kuimarisha mazingira ya michezo skuli, kuongeza ushiriki wa wanafunzi na kuandaa kizazi chenye afya, nidhamu na uwezo wa kuiwakilisha Zanzibar katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.
Imetolewa na kitengo ch Habari, Mawaslisiano na Uhusiano – WEMA.