
Kuimarisha uwezo wa viongozi wa skuli ni miongoni mwa hatua muhimu zinazochangia kuboresha ubora wa elimu, kuongeza ufanisi wa ufundishaji na hatimaye kuinua matokeo ya ujifunzaji kwa wanafunzi.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Walimu Zanzibar, Bw. Othman Omar Othman, wakati akichangia mjadala kuhusu nafasi ya uongozi wa skuli katika maendeleo ya sekta ya elimu, uliofanyika katika Wiki ya Ushiriki wa Viongozi wa Shule Tanzania jijini Dar es Salaam.
Bw. Othman amesema Serikali inaendelea kuipa kipaumbele ajenda ya kuimarisha uongozi wa skuli, ikitambua kuwa viongozi wenye uwezo wa kitaaluma ni chachu ya maboresho katika usimamizi wa skuli, maendeleo ya walimu na ufaulu wa wanafunzi.
Alieleza kuwa viongozi wa skuli wanayo nafasi ya kutoa ushauri elekezi, mwongozo wa kitaaluma na msaada wa kiufundi kwa walimu, hatua inayochangia kuboresha mbinu za ufundishaji na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akisisitiza umuhimu wa uongozi huo, alisema lengo kuu la mfumo wa elimu ni kuhakikisha kila mwanafunzi anapata elimu yenye ubora na kufikia viwango vinavyotarajiwa vya ujifunzaji, huku matokeo ya wanafunzi yakibaki kuwa kipimo muhimu cha mafanikio ya sekta ya elimu.
Aidha, alifafanua kuwa mafanikio ya wanafunzi yanategemea mnyororo unaoanzia kwenye uongozi madhubuti wa skuli, unaowawezesha walimu kufundisha kwa ufanisi zaidi na kuwajengea wanafunzi mazingira bora ya kujifunza.
Aliongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo inaendelea kuwekeza katika kuimarisha uwezo wa viongozi wa skuli kupitia programu mbalimbali za maendeleo ya kitaaluma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kujenga mfumo wa elimu wenye ubora, usawa na matokeo endelevu.
Kupitia uwekezaji huo, Zanzibar inaendelea kuimarisha msingi wa uongozi wa skuli unaolenga kuongeza ubora wa elimu, kuimarisha utendaji wa taasisi za elimu na kuwaandaa wanafunzi wenye maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya maendeleo ya taifa.