
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Lela Muhamed Mussa amewataka wakandarasi wanaojenga majengo ya skuli kuhakikisha wanazingatia viwango vya ubora katika miundombinu ya majengo hayo hasa miundombinu ya zimamoto ili kuepusha majanga wakati wa matumizi ya majengo hayo.
Amesema hayo leo tarehe 6 Julai 2026 katika ziara ya kufatilia maendeleao ya miradi ya ujenzi wa skuli Mtoni kidatu (Chemchem) na Kianga Mkoa wa Mjini Magharibi- Unguja.
Mhe Lela amesema ujenzi huo unalengo la kuendelea kupunguza changamoto ya wingi wa wanafunzi katika Madarasa, hivyo ni vyema kukamilika kwa wakati ili Watoto wasome katika mazingira mazuri na salama.

Nae Sheha wa Mtoni kidatu ndugu Mukki Makkame Ussi amemuhakikishia waziri kuwa atafuatilia ujenzi huo hatua kwa hatua ili ukamilike kwa wakati.
Mkandarasi kutoka kampuni ya Til construction limited Ndugu Bernard Limo amesema ujenzi wa skuli ya msingi Mtoni kidatu ni wa ghorofa 3 (G+ 3), ambao utakua na Madarasa 46 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 200 na kwa sasa ujenzi upo kwenye hatua ya asilimia 18, wakati ujenzi wa skuli ya Kianga umefikia aslimia 24 na utakua na Madarasa 40.
Mapema mshauri elekezi kutoka kampuni ya Mhandisi Ndugu Godfrey Augost Kessy amesema kwa kushirikiana atahakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kiwango bora na salama.
Katika ziara hiyo viongozi mbali mbali wa wizara na shehia walishiriki katika ziara hiyo ambopo walitembelea ujenzi wa skuli ya Kianga na Mtoni Kidatu (Chemchem).
Imetolewa na kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano –(WEMA)