
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ndg. Khamis Abdulla Said, amehitimisha rasmi utekelezaji wa Mradi wa Zanzibar Digital Education uliotekelezwa na Kampuni ya eeeAustria International Projects GmbH ya Austria kupitia mkopo nafuu kutoka Serikali ya Austria.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mradi huo iliyofanyika leo, tarehe 03 Julai 2026, Katibu Mkuu aliwataka watendaji wa Wizara pamoja na wadau wa elimu kuendelea kutumia na kuendeleza ujuzi walioupata kupitia mafunzo yaliyotolewa na mradi huo ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.

Aidha, alieleza kuwa Wizara imenufaika kwa kiwango kikubwa kupitia mradi huo, ambapo skuli 33 zimepatiwa vifaa vya kisasa vya TEHAMA kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia. Hatua hiyo inatarajiwa kuboresha mazingira ya elimu na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika madarasa.
Katibu Mkuu pia alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miundombinu na vifaa vilivyowekezwa vinatunzwa na kutumika ipasavyo ili kuleta matokeo chanya na endelevu katika sekta ya elimu Zanzibar.
Mradi wa Zanzibar Digital Education umesimamiwa na Idara ya TEHAMA katika Elimu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, ukiwa na lengo la kuimarisha ubora wa elimu kupitia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Uhusiano, WEMA.