
Walimu wakuu wametakiwa kuwasimamia walimu wanaowaongoza ili kuhakikisha kuwa upimaji wa wanafunzi unafanyika katika muda unaokubalika ili kutambua maendeleo ya mwanafunzi katika kujifunza pamoja na kuweza kuwasaidia ili kufikia malengo ya mitaala katika ngazi husika.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu taaluma Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt Mwanakhamis Adam Ameir leo tarehe 22 Juni 2026 alipofungua Kikao Kazi kilichoandaliwa na Kitengo cha Uratibu wa skuli binafsi katika ukumbi wa Skuli ya sekondari ya Lumumba Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Aidha, Dkt Mwanakhamis amewabainishia walimu hao kuwa endapo wanafunzi watatayarishwa ndani ya muda hakutakuwa na haja ya skuli kuweka kambi badala yake skuli ibuni mikakati maalumu ambayo itawasaidia watoto kufaulu kwa kiwango kinachokusudiwa.
Akizungumza kuhusu mahafali, Dkt Mwanakhamis amesema kuwa mahafali ni Sherehe za kitaaluma hivyo nl budi sherehe hizo zifanywe kwa makusudio ya kitaaluma sambamba na kuzingatia mila, silka na Utamaduni unaokubalika katika jamii yetu.
Kwa upande wake Dkt Halima Ali Ahmada ambaye ni mkuu mpya wa Kitengo cha Uratibu wa skuli binafsi alitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa walimu hao na kuwaomba kumpa mashirikiano katika kufanikisha vyema majukumu ya kila siku na kuekeza kuwa anatambua mchango mkubwa unaotolewa na Skuli hizo katika kuchangia maendeleo ya sekta ya elimu nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Kamisheni ya Kazi Ndugu Ali Hamdani Bakari amewataka walimu wakuu wa Skuli binafsi kufuata maelezo yaliyotolewa na kamisheni ya kazi hususan katika suala la ulipaji wa mishahara kwa walimu wa skuli hizo na kwasisitiza walimu wakuu kufika Wizarani kwa ajili ya kuchukua mikataba husika.
Naye, Meneja wa Mtaala na Usimamizi wa vifaa, Ndg Wanu Ali Makame ameeleza kuwa mihutasari ni katika vifaa muhimu katika utekelezaji wa mitaala katika elimu na kutoa ushauri kuwa kwenda sambamba na muda ulioainishwa katika mihutasari kutaondoa ulazima wa kuweka kambi pamoja na kuweka mazingira rafiki ya kujifunza kulingana na uwezo na kiwango cha wanafunzi.
Kwa upande mwengine, Afisa Juma Salim Ali amewataka walimu wakuu wa Skuli binafsi kuangalia kwa upana ushiriki na uwezo wa watoto wenye mahitaji maalum na kutokutumia sababu hizo kumkaririsha darasa mwanafunzi wa aina hiyo kwa kisingizio cha kupata alama kidogo bila ya kuzingatia hali aliyonanayo mtoto huyo.
Kikao kazi hicho kimewashirikisha walimu wakuu wa Skuli binafsi kutoka Wilaya za Kaskazini A na B pamoja na Wilaya ya Magahribi A.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.