
Juni 18, 2026
Shirika la Imagine Worldwide limeendelea na maandalizi ya uzinduzi wa Mradi wa Msingi TEK unaotarajiwa kufanyika Zanzibar, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Katika kujiandaa na hafla hiyo, shirika hilo limekutana na watendaji pamoja na wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Uzinduzi kwa lengo la kuendeleza mafunzo ya kufanya mjadala wa pamoja utakaosaidia kufanikisha tukio hilo muhimu. Mkutano huo uliofanyika katika hoteli ya Madinatul Bahar Mbweni Mjini Zanzibar, pia umelenga kuwajengea uelewa zaidi washiriki kuhusu majukumu yao katika maandalizi na utekelezaji wa shughuli za uzinduzi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Imagine Worldwide, Dkt. Jacqueline Halim Mgumia, amesema kuwa maandalizi yote yanaendelea vizuri na kwamba taratibu mbalimbali zinazohitajika kwa ajili ya uzinduzi huo zinaendelea kukamilishwa kwa wakati ili kuhakikisha tukio hilo linafanikiwa kama ilivyopangwa.
Aidha katika kikao hicho washiriki walipewa muhtasari wa hali ya mahudhurio ya wanafunzi katika skuli zinazotekeleza programu ya Msingi TEK Zanzibar. imeelezwa kuwa mahudhurio ya wanafunzi ni mazuri ambayo yanaonesha mwitikio chanya wa jamii katika programu hiyo.
Hata hivyo, imebainishwa kuwa changamoto ya uingiaji wa wanafunzi katika awamu ya mchana katika baadhi ya skuli inapunguza muda wa kujifunza kwa wanafunzi, jambo ambalo linahitaji kuangaliwa ili kuhakikisha wanafunzi wanapata muda wa kutosha wa kujifunza na kunufaika kikamilifu na programu hiyo.
Washiriki wa mkutano huo walipata fursa ya kujadili mikakati mbalimbali ya kuhakikisha uzinduzi wa Mradi wa Msingi TEK unafanyika kwa mafanikio makubwa na kuendelea kuimarisha ubora wa elimu kwa kutumia teknolojia katika skuli za Zanzibar.
Imetolewa na Kitengo cha Habari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar.