
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu Khamis Abdulla Said amesema serikali kwa kushirikiana na mashirika mbali mbali imekuwa ikihakikisha wanasimamia vyema na kuimarisha sera ya elimu ikiwemo elimu mjumuisho.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa makubaliano (MoU) baina ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na Shirika la watu wenye ulemavu la Norway (NAD) leo tarehe 12 June 2026 Katibu Khamis amesema hatua hiyo inalengo la kuleta mabadiliko mazuri kwenye jamii hasa katika kuwawezesha na kuzilinda haki za watu na wanafunzi wenye ulemavu nchini.
Amesema mkataba huo unajenga misingi imara wa ushirikiano ambapo unaenda kutekeleza katika maeneo mbali mbali ikiwemo kuendeleza na kuimarisha mkakati na sera jumuishi ili kuhakikisha mifumo ya elimu inakidhi mahitaji ya wanafunzi wote bila ya ubaguzi.
Aidha amefahamisha kuwa mkataba huo pia utazingatia utoaji wa mafunzo ya elimu mjumuisho kwa walimu katika wilaya zote 11 za Unguja na Pemba ili kuwapatia mbinu na ujuzi wa kisasa wa kufundisha, pamoja na kupatiwa vifaa vya kisasa watoto wenye ulemavu vya kujifunzia.
Imetolewa na kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano- (WEMA)