
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu Khamis Abdulla Said amesema Serikali inachukua jitihada mbali mbali katika kukuza na kuwaendeleza watu wenye ulemavu katika sekta mbali mbali ikiwemo ya Elimu, pamoja na kuzingatia haki zao ili waweze kutimiza malengo yao.
Ameeleza hayo leo tarehe 11 June 2026 wakati akizundua Kamati ya ushauri ya elimu mjumuisho Zanzibar, pamoja na kikao cha pili cha kamati hiyo huko katika ukumbi wa mikutano Michenzani Mall, Mkoa wa mjini Magharibi Unguja.
Amesema hatua hizo ni pamoja na kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwapatia elimu watoto wenye ulemavu ambapo kumekuwa na ongezeko la watoto wenye ulemavu mwaka hadi mwaka kutokana na serikali kuimarisha mazingira pamoja na kuzingatia mahitaji yao katika miundombinu mbali mbali wanayoijenga.
Katibu Khamis amefahamisha kuwa kamati hiyo inajukumu la kuweka msingi imara, kuandaa mpango kazi na kufanya tathmini ya kina na ya hali ya elimu mjumuisho katika skuli zote za visiwa vya Zanzibar, jukumu jengine ni kuandaa programu za mafunzo endelevu kwa walimu, wazazi na jamii kuhusu watu wenye mahitaji maalum.
Nae Naibu katibu mkuu Utawala wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu Amos John Henock amesema wizara itaendelea kushirikiana na taasisi na wadau mbali mbali katika kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata haki yao ya elimu na kutimiza ndoto zao kama walivyo wengine.
Imetolewa na kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano- (WEMA)