
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khadija Salum Ali, tarehe 8 Juni 2026 ameshiriki katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la jengo la Open University of Tanzania (OUT) Tawi la Pemba, lililopo Vitongoji, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.
Mhe. Khadija ameshiriki hafla hiyo akimuwakilisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkuu wa Chuo hicho, Mizengo Kayanza Pinda, ambaye aliweka jiwe la msingi kuashiria mwanzo wa utekelezaji wa mradi huo muhimu wa maendeleo ya elimu kisiwani Pemba.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Pinda amesema ujenzi wa tawi hilo la OUT utasaidia kuongeza fursa za elimu ya juu kwa wananchi wa Pemba na Zanzibar kwa ujumla, sambamba na kuimarisha maendeleo ya kitaaluma na kijamii.
Aidha, Naibu Waziri Mhe. Khadija Salum Ali amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za elimu katika kuimarisha mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu yenye ubora na inayokidhi mahitaji ya wakati.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa elimu, wananchi pamoja na wanafunzi kutoka maeneo tofauti ya Pemba.