
04 Juni, 2026
Chuo cha Ualimu Nkrumah – Unguja
Manaibu Katibu Wakuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Mwanakhamis Adam Amer na Ndg. Amos Enock John, wamefanya ziara ya kutembelea Chuo Kikuu cha Nkrumah kilichopo Mfenesini, Unguja.
Ziara hiyo ilihusisha kikao kazi cha kutengeneza na kupitia kwa kina mihtasari ya masomo kwa lengo la kuimarisha ubora wa elimu na kuweka msingi madhubuti wa mabadiliko ya mfumo wa elimu, ikiwemo hatua ya kuliondoa Darasa la Saba.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Taaluma, Dkt. Mwanakhamis Adam Amer, aliwasisitiza wadau wote kuuzingatia mtaala huo kwa kuwa ni mali ya jamii nzima.
Aidha, aliwashukuru wadau wote waliokubali kutoa muda wao kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Zanzibar katika kazi hiyo muhimu iliyodumu kwa siku nane.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utawala, Ndg. Amos Enock John, alisema kuwa lengo kuu la mapitio hayo ni kumsaidia mwanafunzi kupata elimu bora inayozingatia mtaala na kuendana na mabadiliko ya wakati.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu ya Zanzibar, Ndg. Abdalla M. Mussa, alisema kuwa kikao kazi hicho kimewashirikisha walimu wabobezi wastaafu pamoja na wataalamu kutoka vyuo vikuu na vyuo vya kati, kwa lengo la kuimarisha na kuboresha mihtasari hiyo.
Ameedelea pia kuwashukuru wataalamu hao kwa ushiriki wao mkubwa na kwa kukubali kutenga muda wao ili kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Zanzibar katika kufanikisha hatua hiyo muhimu ya kuboresha elimu nchini.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Uhusiano (WEMA).