
04 Juni, 2026
Wilaya ya Magaribi “A” – Unguja
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ndugu Amos John Henock, amefanya ziara ya kushtukiza katika Skuli ya Sekondari Mwenge na Langoni zilizopo Mkoa wa Mjini, Wilaya ya Magharibi “A”, Unguja.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kuzungumza na wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mitihani ya taifa kwa kuwahamasisha kufanya vizuri katika masomo yao ili kuleta matokeo chanya yatakayoiwezesha skuli hiyo kuendelea kufanya vizuri katika viwango vya ufaulu.
Aidha, aliwataka wanafunzi kutumia elimu watakayopata kama nyenzo ya kuwawezesha kuajiriwa au kujiajiri kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.
Katika mazungumzo yake, Ndugu Amos John Henock aliwasisitiza wanafunzi kuwa makini katika kutekeleza malengo waliyojiwekea, pamoja na kutumia vyema muda wao wa ziada kwa kujisomea na kufanya maandalizi ya mitihani.
Halikadhalika, aliwahimiza kujiepusha na vishawishi mbalimbali vinavyoweza kujitokeza katika mazingira yao ya kila siku na kuathiri maendeleo yao ya kielimu.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar za kuendelea kufuatilia na kuimarisha kiwango cha elimu pamoja na ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya taifa.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Uhusiano (WEMA).