
Viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar wamekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu la Finland pamoja na maafisa kutoka Ubalozi wa Finland nchini Tanzania katika ofisi za Wizara ya Elimu Mazizini, Unguja.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo tarehe 25 Mei, 2026 yakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ndugu Khamis Abdulla Said, pamoja na Naibu Katibu Mkuu Taaluma, Dkt. Mwanakhamis Adam Ameir, katika ofisi ya Naibu Katibu Mkuu Taaluma.

Ujumbe huo umefika kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa programu ya mafunzo ya amali jumuishi inayotekelezwa katika Kituo cha Vijana Wenye Ulemavu wa Akili cha Jang’ombe.
Programu hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Shirika la Watu Wenye Ulemavu wa Akili la Finland (FAIDD), pamoja na Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu wa Akili Zanzibar (ZAPDD).
Kupitia programu hiyo, vijana wenye ulemavu wa akili wanapatiwa mafunzo ya amali yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Imetolewa na Kitengo cha habari na Uhusiano (WEMA).