
Kuwa na Utamaduni wa kuwaenzi wasanii wa kale ni kuwaonesha thamani ya kazi zao katika taifa.
Hayo ameyasema Waziri wa elimu na mafunzo ya amali Zanzibar mhe Lela Muhamed mussa kwa niaba ya mke wa rais wa Zanzibar mama nariyam mwinyi katika Ukumbi wa Sun Shine Hall, uliopo Chukwani Buyu nje kidogo ya Mji wa Zanzibar,
Mheshimiwa Lela alieleza kuwa serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na Bi Rukia Ramadhan katika kuendeleza sanaa ya Taarab, ambayo ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Zanzibar.

Alisisitiza umuhimu wa kuenzi wasanii wakongwe wakiwa hai na hata baada ya mchango wao, ili vizazi vijavyo viweze kujifunza na kuendeleza urithi huo wa kiutamaduni.
Aidha, alibainisha kuwa tukio hilo la Shukurani ya Bimkubwa si tu kumbukumbu ya heshima kwa msanii huyo, bali pia ni jukwaa la kuhamasisha jamii kuthamini sanaa na wasanii wake.
Alitoa wito kwa vijana kujifunza kutoka kwa wakongwe hao ili kulinda na kuendeleza utamaduni wa Zanzibar.
Kwa upande wao, wasanii na washiriki wa hafla hiyo walieleza kuguswa na heshima hiyo waliyopewa Bi Rukia Ramadhan, wakisema kuwa mchango wake umeacha alama kubwa katika tasnia ya muziki wa Taarab. Burudani ya muziki huo ilitawala hafla hiyo, huku nyimbo mbalimbali za asili zikiimbwa kuadhimisha maisha na kazi ya msanii huyo mkongwe.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa utoaji wa tuzo na zawadi maalum kwa Bi Rukia Ramadhan kama ishara ya shukrani na kuthamini mchango wake katika sanaa ya muziki wa Taarab Zanzibar.
Imetolewa na kitengo cha habari na uhusiano
WEMA.
2026
