
Bajeti ya makadirio ya matumizi na mapato ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2026/2027 imepitishwa na wajumbe wa Baraza la wawakilishi.
Awali akiwasilisha bajeti hiyo huko katika kikao cha Baraza la wawakilishi Waziri wa wizara hiyo Mhe Lela Muhamed Mussa amesema kwa mwaka wa fedha 2026/2027 wizara imekadiria kutumia shilingi 1,100,488,057 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.
Mhe Lela amesema wizara katika bajeti hiyo imepanga kutekeleza vipaombele sita ikiwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa elimu bora katika ngazi ya elimu ya lazima na kuimarisha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji.
Mhe Lela amevitaja vipaombele vyengine kuwa ni kutanua na kuimarisha elimu ya mafunzo ya amali na ufundi kwa kuzingatia soko la ajira, kuimarisha matumizi ya TEHAMA na mifumo ya kidijitali, kuimarisha upatikanaji wa fursa za elimu ya juu na kuimarisha usimamizi wa uongozi wa sekta ya elimu.
Wakiichangia bajeti hiyo wajumbe wa Baraza la wawakilishi wametoa maoni, Ushauri na michango yao juu ya kuimarisha utekelezaji wa wizara hiyo na wameipongeza serikali kwa juhudi inazozichukua katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Imetolewa na Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano – WEMA