
Mkurugenzi Idara Elimu Sekondari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu Asya Iddi Issa amewataka wanafunzi wa michepuo ya kilimo Skuli ya Sekondari Mikindani kuzingatia umuhimu wa utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya tabianchi.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Sekondari wa skuli hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi eneo la kilimo baada ya kufanyiwa maboresho na UNICEF kupitia mradi wa kuhifadhi mazingira huko Dole Mikindani Wilaya ya Magahribi A Unguja.
Ameeleza kuwa wanafunzi wa kilimo wanapaswa kutumia maarifa yao ili kuendeleza kilimo endelevu kinacholinda mazingira, ikiwa ni pamoja na matumizi bora ya maji, uhifadhi wa udongo, pamoja na kuongeza uzalishaji wa mazao ili kuhakikisha usalama wa chakula nchini.
Akizungumzia suala la uchakataji wa taka, Mkurugenzi Asya amesisitiza umuhimu wa kurejeleza taka na kuzitumia kama mbolea ya asili, hatua itakayosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza rutuba ya udongo.
Aidha, amehimiza upandaji wa miti na matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira, jambo ambalo litachangia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa muda mrefu.
“Hafla hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha elimu ya vitendo kwa wanafunzi ili kujenga taifa lenye uelewa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kimazingira pamoja na kuondoa utegemezi wa ajira.
Imetolewa na Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano WEMA