
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kupitia Kitengo cha Elimu Mjumuisho na Stadi za Maisha imefanya zoezi la upimaji wa afya kwa wanafunzi walioanza masomo katika skuli za maandalizi, ikiwa ni jitihada za kuwawezesha kujifunza kwa ufanisi.
Zoezi hilo limefanyika leo, Februari 11, 2026, katika Skuli ya Maandalizi Bwejuu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Akizungumza baada ya zoezi hilo, Afisa Elimu Jumuishi, Bi. Zuena Mohammed Nassor, amesema kuwa upimaji huo una lengo la kubaini changamoto za kiafya kwa wanafunzi hao na kuzitafutia ufumbuzi mapema kabla ya kuanza rasmi mchakato wa kujifunza.
Ameeleza kuwa katika hatua ya majaribio, zoezi hilo linatekelezwa katika skuli tisa (9) za Unguja na skuli tisa (9) za Pemba. Amesema Wilaya ya Kaskazini A tayari imeshafikiwa, na zoezi linaendelea katika Wilaya ya Kusini na kuelekea kukamilika katika Wilaya ya Mjini pamoja na Magharibi B.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Afya aliyeshiriki katika zoezi hilo, Dkt. Mwanakhamis Ali Abdalla, amesema vipimo vilivyofanyika ni pamoja na uchunguzi wa viungo, usikivu, uoni, afya ya akili pamoja na ngozi.
Amefafanua kuwa watoto wengi wameonekana kuwa na changamoto ya usikivu kutokana na mrundikano wa taka masikioni, na tayari wanaendelea kupatiwa matibabu ili waweze kuwa na uwezo mzuri wa kupokea na kuelewa masomo darasani.
Kwa upande wao, wazazi wa wanafunzi hao wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuanzisha mpango huo, wakisema umeisaidia familia nyingi kutambua mapema changamoto za kiafya za watoto wao na kupata matibabu stahiki bila gharama kubwa.
Imetolewa na Kitengo cha Habari Mawasiliano na Uhusiano (WEMA).