Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar (VTA) leo imepokea ugeni kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar kwa ajili ya kutoa mafunzo kuhusu mfumo wa usimamizi wa mali za Serikali unaojulikana kama ZGAMIS (Zanzibar Government Asset Management Information System).
Mafunzo hayo yanayotarajiwa kufanyika kwa muda wa siku tatu yanaendeshwa katika Ukumbi wa Ofisi Kuu za VTA zilizopo Malindi. Wakufunzi wa mafunzo hayo ni Ndugu Suleiman Mohammed Bakari, Msimamizi wa Mali kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, pamoja na Ndugu Munira Haji Hamza, Msimamizi wa Mali na Hazina Zanzibar.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Ndugu Suleiman Mohammed Bakari ambaye ni mkufunzi mkuu, alieleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo washiriki katika kuelewa na kusimamia mali za Serikali kwa kuzingatia miongozo na taratibu rasmi za Serikali kupitia mfumo wa ZGAMIS.
Alisisitiza kuwa kila mtumishi wa Serikali ana wajibu wa kutumia, kusimamia na kutunza mali za umma kwa uadilifu na umakini ili kuhakikisha zinadumu na kuwa na ubora unaotakiwa. Aidha, alibainisha kuwa mali zote za Serikali zinapaswa kusajiliwa katika mfumo huo kabla ya kuanza kutumika rasmi.
Kwa upande wake, alikumbusha kuwa usajili sahihi wa mali za umma katika mfumo wa ZGAMIS ni hatua muhimu ya kuimarisha uwajibikaji, uwazi na usimamizi bora wa rasilimali za Serikali.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuendelea kesho tarehe 12 Februari 2026 kwa kuzingatia ratiba iliyopangwa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Uhusiano Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Tarehe 11 Februari 2026.