Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt Bakari Ali Silima Akipokea Tuzo ya Ubunifu katika Sekta ya Umma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar (VTA), Dkt. Bakari Ali Silima, amepokea tuzo ya ubunifu katika sekta ya umma, iliyotolewa kwa kutambua mchango na juhudi za VTA katika kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu kupitia elimu ya ufundi na mafunzo ya amali.
Tukio la kukabidhi tuzo hiyo limefanyika tarehe 31 Januari 2026, ambapo Dkt. Bakari Ali Silima alipokea tuzo hizo akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Mafunzo na Miongozo wa VTA, Ndugu Ghaitha Gharib Masoud.
VTA imetangazwa mshindi wa ubora katika maeneo matatu muhimu ambayo ni Elimu ya Ufundi, Maendeleo ya Ujuzi, pamoja na Uwezeshaji wa Nguvu Kazi, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa sera, mipango na mikakati bunifu inayolenga kuongeza ujuzi kwa vijana na jamii kwa ujumla.
Tuzo hizo zimetolewa na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kama sehemu ya kutambua taasisi za umma zinazotekeleza majukumu yao kwa ubunifu, ufanisi na mchango chanya katika maendeleo ya taifa.
Kupatikana kwa tuzo hiyo ni ishara ya dhamira ya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar kuendelea kuboresha mifumo ya mafunzo, kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza uchumi na ajira kwa wananchi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano Mamlaka ya Mafunzo Amali Zanzibar
Tarehe 2 Februari, 2026.