
Mkurugenzi Idara ya Elimu Maandalizi na Msingu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bi. Fatma Mode Ramadhan amewataka Walimu kuwa makini na kubuni mikakati imara katika matumizi ya fedha za ruzuku zinazotolewa na Wizara ya Elimu ili kufanikisha mipango ya maendeleo ya skuli hizo.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Walimu Wakuu pamoja na washika fedha wa skuli za Maandalizi na Msingi katika Mkutano wa kufanya tathmini ya maendeleo na kupanga mikakati mipya ya mwaka, mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa skuli ya msingi ya Dkt. Samia humo Mwanakwerekwe Wilaya ya Magahribi B. Unguja.
Amesema Walimu ni vyema kujikinaisha na kuepukana na matumizi mabaya ya fedha pamoja na uchangishaji holela wa fedha kwa wanafunzi badala yake amewataka kuweka mikakati madhubuti ili kuzitumia vyema fedha za ruzuku katika kuleta maendeleo ya skuli hizo.
Amebainisha kuwa sio jukumu la Wizara kuchunguza ni wapi invoice imetoka, kilichomuhimu ni uhalali wake na kile kilichoainishwa kiwe kina mnasaba na mahitaji ya skuli husika na kuendana na mpango wa ruzuku hizo
Akizungimzia suala la uwekaji wa kambi Mkurugenzi Bi. Fatma amesema suala la uwekaji wa kambi lipo na linakubalika kwa utaratibu uliowekwa lakini amewasisitiza walimu kusimamia vyema ufundishaji kwa kuutumia muda vizuri ili kuepusha ulazima wa kuweka kambi, na hivyo kupunguza mzigo katika ufundishaji.
Awali Akitoa Elimu kwa washika fedha wa skuli, Afisa Muwasilishaji kutoka afisi za Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi (ZAECA) amesema kutokulifahamu kosa hakutoi msamaha kwa aliyetenda kosa hilo, hivyo amewataka walimu hao kujiepusha na makosa ya rushwa ambayo yanahujumu uchumi wa nchi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano na Uhusiano,
WEMA.