
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imeamua kuinua masomo ya sanaa hasa ya Kiswahili, Dini na Kiarabu ili kuendana na mtaala mpya pamoja na mabadiliko yanayoendelea duniani.
Hayo yameelezwa leo tarehe 29 Januari 2026, na Mkurugenzi Idara ya Elimu Sekondari Bi Asya Iddi Issa wakati akifungua mafunzo kwa walimu wa sekondari wa somo la Kiswahili na Dini katika Kituo cha Walimu (TC) Kiembesamaki – Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Amesema mafunzo hayo yatamjengea mwalimu umahiri wa kufundisha, na kuwa mbunifu katika kuwasilisha mada zake kwa vitendo na nadharia.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mafunzo ya Ualimu Bw. Mohammed Khamis Suleiman amesema vituo vya Ualimu vinalenga kumuendeleza mwalimu ili aendane na wakati katika kazi zake, na ameeleza kuwa wameamua kutoa mafunzo hayo kwa sasa kutokana na kutopewa kipaumbele kwa muda mrefu.
Naye Afisa Mshauri wa masomo ya Dini na Kiarabu Bibi Asha Haji Mkema amesema somo la Dini ni somo mama ambalo humjenga mwanafunzi kimaadili katika fani zote ili aendelee vizuri katika masomo yake na jamii kwa ujumla, na amefahamisha kuwa somo la Kiarabu litamuwezesha mwanafunzi kupata ajira sekta mbali mbali duniani.
Nao walimu waliopatiwa mafunzo hayo wameelezea faraja yao baada ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuona umuhimu na thamani yake katika jamii, na wameomba mafunzo hayo yaendelee kutolewa ili na wao waendane na wakati katika kufundisha.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Mawasiliano na uhusiano (WEMA)
Zanzibar.