
Naibu Katibu Mkuu Taaluma Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dr. Mwanakhamis Adam Ameir, amesema ubora wa kuwashughulikia watoto yatima ni mkubwa hivyo ameitaka Jumuiya ya misaada ya TAQWA kuendeleza harakati zao za kutoa misaada ili kuwaletea furaha watoto yatima na wenye mazingira magumu.
Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa vifaa vya skuli kwa Watoto yatima hapo kwenye ukumbi wa skuli ya Haile Selassie Dr. Mwanakhamis amesema kuwa yatima ni Moja Kati ya sifa ya Mtume Muhammad S.A.W hivyo amewataka watoto hao kujisikia furaha na kusoma kwa bidii.
Aidha Dr. Mwanakhamis amewataka wazazi na walezi kuwalea vizuri watoto hao ili kupata baraka kutokana na kuwalea vizuri watoto yatima.
Amesema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar inachukulia kwa uzito mkubwa suala la watoto wenye mazingira magumu na watoto yatima, hivyo ameitaka Jumuiya ya TAQWA kuorodhesha majina ya watoto wote wanaowahudumikia ili Wizara iwaandalie mazingira mazuri ya kielimu watoto hao.
Nae Mwenyekiti wa Taasisi ya Mfuko wa watoto Yatima Tanzania (TAQWA) Mhandisi Salha Mohammed Kassim amesema Taasisi Yao imeamua kuwasaidia watoto yatima kutokana na simulizi ya Sira ya Mtume Muhammad S.A.W juu ya suala la kuwasaidia watoto Yatima na malezi Bora ya watoto.
Ameongeza kuwa Taasisi ya Taqwa ilianza kazi mwaka 2014 na imejikita katika masuala ya kusaidia watoto kielemu, kimaisha na kimavazi.
Aidha Mhandisi Salha amewataka watu wengine wenye uwezo kuwasaidia watoto yatima ili waweze kuishi katika mazingira mazuri.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wazazi Bibi Fatma Khamis Haji amesema kina mama wanapata ugumu mkubwa katika ulezi wa watoto, hivyo ameitaka jamii kuwaonea huruma wanawake wanapofiliwa na waume zao kwa kuwasaidia ulezi wa watoto yatima kama ambavyo Jumuiya ya TAQWA inavyofanya kwa Watoto wao.
Jumla ya watoto yatima 200 wamepatiwa msaada wa vifaa vya skuli ikiwemo mikoba, viatu, madaftari na vifaa vya masomo vikiwemo peni na penseli.
Imetolewa;
Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano (WEMA)