
Watendaji wa Idara ya Elimu Sekondari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara hiyo Ndg Asya Iddi Issa leo tarehe 10/01/2026 wamefanya kikao maalumu pamoja na walimu wakuu wa Skuli zenye Dakhalia na walimu wa taaluma kwa lengo la kutoa miongozo ya kiutendaji.
Katika kikao hicho kilichofanyika katika Skuli ya Tumekuja Wilaya ya Mjini Unguja, miongozo mbalimbali ilifafanunuliwa ikiwemo nidhamu kwa wanafunzi wa Dakhalia kama vile taratibu na kanuni za mavazi pamoja na kuweka wazi mgawanyo wa wanafunzi katika michepuo tofauti kufuatia mabadiliko ya Elimu nchini kwa upande wa taaluma.
Aidha kikao hicho kimefafanua kwamba kutokana na mabadiliko hayo ya Elimu, wanafunzi wanalazimika kusoma katika mikondo tofauti ikiwemo ile ya Amali na Amali ya Uhandisi na kuwataka walimu hao kuwa mabalozi wazuri kwa Wazazi, Walezi na Jamii kwa ujumla ili dhana halisi ya mabadiliko hayo yaweze kufikiwa kwa ufanisi.
Kwa upande mwengine, walimu wametakiwa kuzitumia rasilimali zilizopo licha ya uhaba wake pamoja na kuwatumia walimu walionao katika skuli zao katika nyanja mbalimbali kitaaluma ili kuziba pengo la walimu wataalamu kwa kuwa mabadiliko siku zote huwa hayakosi changamoto.
Kwa upande wa dakhalia walimu hao wameshauri kuwepo huduma thabiti ya usafiri katika dakhalia hizo ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa dharura ikiwemo kuugua hasa nyakati za usiku.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Uhusiano
(WEMA – Zanzibar).