Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum amesema ujenzi na ufunguzi wa skuli za kisasa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar unaenda sambamba na utekelezaji wa dhamira ya Mapinduzi ya kuhakikisha elimu inatolewa bila ubaguzi na kukidhi mahitaji ya ongezeko la wanafunzi.
Dkt. Mkuya ameyasema hayo leo tarehe 8 Januari, alipofungua Skuli ya Msingi Potoa kwa niaba ya skuli ya Mwera Mtofaani na Vuga Mkadini, hafla hiyo ni katika shamrashamra za maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi, iliyofanyika Potoa, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema kabla ya Mapinduzi, elimu ilikuwa fursa adimu iliyopatikana kwa watu wachache huku Waafrika wengi wakinyimwa haki hiyo, hali iliyoendeleza umasikini wa maarifa na kipato pamoja na kukosekana kwa fursa, na hivyo wananchi kushindwa kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Ameongeza kuwa Mapinduzi yaliyoongozwa na Hayati Abeid Amani Karume yaliifanya elimu kuwa haki kwa kila mtu na kuhakikisha kila Mzanzibari anapata elimu bila ubaguzi wowote, sambamba na kuweka msingi imara wa maendeleo ya rasilimali watu ambayo ni nguzo kuu ya maendeleo ya Zanzibar.
Aidha, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, imeendelea kufanya mageuzi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, huduma za maji safi na salama, pamoja na mageuzi makubwa katika sekta ya elimu yanayoambatana na mabadiliko ya mtaala na uimarishaji wa miundombinu.
Amesema Serikali itaendelea kujenga skuli za ghorofa ili kutumia ipasavyo maeneo ya ardhi, kukidhi mahitaji ya wanafunzi, na kuhakikisha wanafunzi wanaingia skuli kwa awamu moja.
Dkt. Mkuya ametoa wito kwa wazazi kushirikiana na walimu katika kusimamia maendeleo ya wanafunzi na kushiriki vikao mbalimbali, akisisitiza kuwa mafanikio ya mtoto kielimu hayaji kwa msaada wa Serikali pekee. Pia amewataka walimu na wazazi kuwahamasisha watoto kuitunza miundombinu ya skuli hizo ili itumike kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Amepongeza juhudi za Rais wa Zanzibar katika kuleta maendeleo nchini na kuipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kusimamia vyema utekelezaji wa miradi hiyo.
Akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu ujenzi wa skuli hizo, Naibu Katibu Mkuu (Utawala) wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ndg. Amos John Henock, amesema ujenzi ulianza Septemba 2024 na kukamilika Desemba 2025, kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni sita milioni mia sita na hamsini.
Amefafanua kuwa kila skuli imegharimu shilingi bilioni moja milioni mia tano na hamsini, ikiwa na maabara za sayansi, vyumba vya kompyuta, chumba cha mshauri nasaha, ofisi za walimu, vyoo 14 na madarasa 15 yenye uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 675 kwa wastani wa wanafunzi 45 kila darasa.
Kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani pamoja na kupunguza masafa marefu kwa wanafunzi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A Ndugu Rashid Simai Msaraka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kudumisha amani na utulivu, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wananchi katika sekta mbalimbali.
Amesema uboreshaji wa sekta ya elimu ni chachu ya maendeleo endelevu kwa siku zijazo kupitia uzalishaji wa wataalamu mahiri katika fani mbalimbali watakaolinda na kuijenga nchi kwa taaluma na ufanisi, kwa misingi ya maandalizi bora ya elimu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Uhusiano.
WEMA – Zanzibar.