
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imezindua rasmi mradi wa Bridge Tanzania Project wenye lengo la kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri, katika Wilaya ya Kaskazini A, Unguja. Hafla ya uzinduzi wa mradi huo imefanyika leo tarehe 6 Januari 2026 katika eneo la Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mradi huo unatoa mafunzo mbalimbali yakiwemo ufundi wa pikipiki, stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu, ujasiriamali, usindikaji wa mazao pamoja na kuchakata zao la mwani, kwa lengo la kuwajengea vijana ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujiajiri, kuongeza kipato na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza baada ya kuzindua mradi huo, Diwani wa Wadi ya Kidoti Jimbo la Nungwi na Naibu Meya mstaafu wa Wilaya hiyo, Ndg. Twalib Haji Abbas, ameahidi kuwaunga mkono vijana walionufaika na mradi huo kupitia miradi mbalimbali kwa kuwapatia fedha na vitendea kazi, kwa lengo la kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi na kujikwamua na changamoto za ukosefu wa ajira. Aidha, amewataka vijana hao kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakufunzi pamoja na kuwa na juhudi katika fani walizozichagua ili kujijengea uwezo imara.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mtendaji Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dkt. Khamis Khalid Said, amewahimiza vijana hao kuyatumia vyema mafunzo watakayopata ili kuwawezesha kuingiza kipato kwa familia zao na Taifa kwa ujumla. Amefafanua kuwa mradi wa Bridge Tanzania una matarajio makubwa ikiwemo kuwawezesha vijana kupata stadi za kazi zitakazoboresha maisha yao, kuongeza idadi ya watu wenye stadi za msingi pamoja na kuongezeka kwa vikundi vya uzalishaji.

Naye Afisa Elimu wa Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, Ndg. Juma Mwadini Abdalla, ameipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kupitia Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima pamoja na UNESCO kwa kuwasaidia vijana kujiajiri, akisema hatua hiyo itachangia kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar ya kuzalisha ajira zaidi ya laki tatu. Ameongeza kuwa UNESCO ni mkombozi wa vijana na ameonesha matumaini makubwa kuwa mafunzo yatakayotolewa kupitia mradi huo yatawawezesha vijana kujikwamua na umasikini.
Akisoma risala ya uzinduzi wa mradi huo, Mratibu wa Mradi, Mustafa Hambal Issa, amesema mradi huo utadumu kwa kipindi cha miaka mitano ukiwa na awamu tatu kwa kila mwaka, na utekelezaji wake rasmi kwa upande wa mafunzo ulianza tarehe 5 Desemba 2025. Ameeleza kuwa ifikapo mwisho wa mradi huo, jumla ya vijana 900 watanufaika katika Wilaya ya Kaskazini A, Unguja.
Kwa upande wake, mshiriki wa mafunzo hayo, Yussuf Foum Issa, amewashukuru watekelezaji wa mradi huo na kuwaomba waendelee kuwawezesha vijana ili kuwasaidia kujiepusha na vitendo viovu na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Imetolewa na :
Kitengo cha Habari na Uhusiano.
(WEMA – Zanzibar)