
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Serikali itaendelea na ujenzi wa Skuli za kisasa zinazoendana na mtaala mpya wa Elimu, unaolenga kuwaandaa vijana kuweza kujiajiri na kuajiriwa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo tarehe 5 Januari, 2026, wakati wa ufunguzi wa Skuli ya Sekondari Chukwani, kwa niaba ya Skuli ya Sekondari ya Regeza Mwendo na Maungani, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar, hafla iliyofanyika Chukwani, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Amesema ujenzi wa skuli za kisasa, ikiwemo Skuli ya Sekondari Chukwani, umeanzishwa kwa lengo la kuwajenga vijana wenye maarifa, maadili na ubunifu, wanaoweza kuunganisha nadharia na vitendo ili kuwa raia wenye uwezo wa kujitegemea na kuchangia kikamilifu maendeleo ya taifa.

Aidha, amesema Mapinduzi ya Zanzibar yameondoa mfumo wa ubaguzi na kuweka msingi wa Serikali inayohakikisha haki ya elimu kwa wote, hali iliyoifanya Zanzibar kuwa jamii yenye usawa, mshikamano na matumaini ya maendeleo endelevu. Ameongeza kuwa ufunguzi wa skuli hiyo ni mageuzi makubwa ya kielimu na utekelezaji wa falsafa ya Mapinduzi kwa vitendo, akibainisha kuwa kabla ya Mapinduzi Zanzibar ilikuwa na Skuli Tano pekee zenye wanafunzi 1,038.
Waziri Mkuu amepongeza juhudi za Serikali kwa uwekezaji unaoendelea katika sekta ya elimu, akisisitiza kuwa elimu bora ni msingi wa maendeleo endelevu ya taifa, huku akiwahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kutunza miundombinu ya skuli ili itumike kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ndg. Khamis Abdulla Said, amesema ujenzi wa skuli hizo ulianza Mei 2025 na kukamilika Desemba 2025, chini ya Kampuni ya Cook’s Construction Tanzania.

Ameeleza kuwa ujenzi wa Skuli ya Sekondari Chukwani umegharimu shilingi Bilioni 6.1, ikiwa na Ghorofa tatu, madarasa 42, vyoo 52, ofisi za Walimu na Mwalimu mkuu, chumba cha Kompyuta pamoja na maabara za kisasa, na ina uwezo wa kuchukua Wanafunzi 1,890 kwa awamu moja.
Katibu Mkuu huyo amesema ufunguzi wa Skuli hizo umeboresha Mazingira ya elimu kwa kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuondoa changamoto ya mfumo wa mikondo miwili iliyokuwa ikiathiri ratiba ya masomo na mitihani. Amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kutoa kipaumbele kwa sekta ya elimu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mheshimiwa Khadija Salum Ali, amesema Serikali itaendelea kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2026 kwa kujenga miundombinu ya elimu, hususan skuli za kisasa zinazoendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia Unguja na Pemba.
Ametoa shukrani kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushiriki katika kuenzi Mapinduzi ya Zanzibar, akisema hatua hiyo inaonesha uzalendo na kuchangia kuimarisha Muungano wa Tanzania.
Akitoa salamu za ukaribisho, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi amewashukuru viongozi wakuu wa Serikali kwa hekima na busara zao zinazoendelea kudumisha amani na kuleta maendeleo nchini.
Imetolewa na Kitengo cha Habari WEMA.