
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesaini mkataba wa ujenzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Bahari ya SUZA, chini ya Mradi wa Kuwawezesha Vijana Kujiajiri na Kuajirika kupitia Uchumi wa Buluu (SEBEP), leo tarehe 2 Januari 2026 huko Mazizini Mkoa wa Mjini Magharibi.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ndg. Khamis Abdulla Said, amesema Wizara ina matumaini makubwa ya kukabidhiwa mradi huo ukiwa na viwango vya kimataifa, kulingana na masharti ya mkataba.
Amesema Wizara itahakikisha inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mkataba huo kwa kuzingatia vigezo vyote vilivyokubaliwa, ikiwemo muda wa utekelezaji wa miezi 18, ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa ufanisi.
Aidha, amesema Wizara imetoa kipindi cha miezi mitatu kuanzia tarehe ya kusaini mkataba, kwa mkandarasi kuwasilisha maombi ya rasilimali zitakazohitajika, ikiwemo vifaa vya ujenzi na wataalamu, kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa mradi huo.
Amefafanua kuwa ujenzi wa Taasisi hiyo unatarajiwa kuwa wa kisasa na utajumuisha jengo la utawala (Administration), madarasa ya kufundishia kwa vitendo, karakana ya mafunzo ya kuzima moto na huduma za ubaharia, jengo la mafunzo ya kuendeshea meli (bridge simulator), pamoja na sehemu ya kuogelea (swimming pool).
Katika kutekeleza azma ya Mradi wa SEBEP, Katibu Mkuu Khamis amewataka wakandarasi wa kampuni ya M/s TIL Construction Limited kuwaajiri vijana wa ndani ya Zanzibar wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Akitoa muhtasari wa mchakato wa manunuzi ya zabuni ya ujenzi, Meneja wa Mradi wa SEBEP, Ndugu Salum Mkubwa Abdulla, amesema zabuni ya mradi huo ilitangazwa tarehe 28 Julai 2025, ambapo jumla ya kampuni 21 zilinunua nyaraka za zabuni. Hatimaye, kampuni ya M/s TIL Construction Limited ilishinda zabuni hiyo kwa gharama ya 9,167,458,454.1/-
Kwa upande wake, Mkandarasi wa kampuni ya M/s TIL Construction Limited, Ndugu Faraji Selemani, ameishukuru Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa kuipa kampuni hiyo fursa ya kutekeleza mradi huo na kuahidi kuutekeleza kwa ufanisi na kwa mujibu wa mkataba.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Uhusiano WEMA.