Rais mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohammed Shein, amesema kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yanapaswa kuheshimiwa na kuenziwa kwani ndiyo chachu ya maendeleo ya elimu yanayopatikana Zanzibar.
Dkt. Shein ameyasema hayo leo tarehe 31 Desemba 2025 alipozindua dakhalia katika Skuli ya Sekondari ya Mikindani Dole, kwa niaba ya dakhalia ya Lumumba, Misufini na Paje Mtule, huko Dole Mikindani, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema Mapinduzi yaliweka msingi imara wa upatikanaji wa haki za msingi, hususan elimu, hivyo ni muhimu kuyapa kipaumbele na kuwashukuru waasisi wa Mapinduzi hayo chini ya uongozi wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali katika kuandaa mikakati na kutekeleza miradi ya ujenzi wa dakhalia hizo, akisema kuwa ni mageuzi makubwa ya kielimu ambayo hayakuwepo wakati wa ukoloni.
Dkt. Shein amefahamisha kuwa elimu ni sekta muhimu katika nchi yoyote kwani ndiyo inayozalisha wataalamu wa fani mbalimbali na kuleta maendeleo ya taifa. Vilevile, amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya kuboresha elimu kupitia ujenzi wa miundombinu ya dakhalia kwa maendeleo ya wanafunzi.
Akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu ujenzi wa dakhalia hizo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ndg Khamis Abdalla Said, amesema ujenzi wa dakhalia hizo umehusisha majengo ya wanafunzi wa kike na wa kiume, ambapo ujenzi ulianza mwezi Septemba 2024 na kukamilika Disemba 2025.
Amesema kila dakhalia imegharimu shilingi bilioni 1.58, huku jengo la jiko la kisasa na sehemu ya kulia chakula likigharimu shilingi milioni 278. Ameongeza kuwa kila dakhalia ina vyumba 12, vitanda na magodoro, vyumba vya wasimamizi wa wanafunzi, sehemu 14 za kuogea, na zina uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 272.
Dakhalia hizo zimejengwa kufuatia ongezeko kubwa la ufaulu wa wanafunzi wa Darasa la Saba pamoja na lengo la kupunguza changamoto kwa wanafunzi wenye hali ngumu za kimaisha kutoka mijini na vijijini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mheshimiwa Khadija Salum Ali, amesema ufunguzi wa dakhalia hizo ni ushahidi wa matunda ya Mapinduzi na hatua muhimu ya maendeleo ya sekta ya Elimu nchini. Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwaletea wananchi maendeleo katika sekta mbalimbali.
Akitoa salamu za Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkuu wa Mkoa huo Ndg Mohamed Ali Abdalla amempongeza Rais wa Zanzibar pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kudumisha amani na kuendelea kuwapambania wananchi kupata maendeleo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano WEMA