Naibu Katibu Mkuu Taaluma Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt Mwanakhamis Adam Ameir ameipongeza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ya Tanzania bara kwa jitahada za makusudi ya kutekeleza ahadi ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizozitoa katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi katika sekta mbalimbali ikiwemo ya Elimu nchini.
Pongezi hizo amezitoa leo tarehe 30 Disemba 2025 katika ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi, Wilaya ya Mjini alipofungua warsha maalum ya siku moja ya kukusanya maoni kuhusu mpango wa Mafunzo linganishi kwa Wanafunzi wa VETA na Vyuo Vikuu.
Dkt Ameir amebainisha kuwa kupitia ahadi hiyo ya Mhe Rais imeonekana kuwa kuwa kuna pengo kubwa kati ya Mafunzo yanayotolewa katika taasisi zetu za kielimu na soko la ajira na au ujuzi ambao waajiri wanaouhitajia katika maeneo yao ya kazi.
Aidha, Dkt. Ameir amewataka washiriki hao kuzihudhurisha akili na fikra zao kwa umakini mkubwa wakati wakisikiliza uwasilishaji huo ili kuweza kujua ni maeneo gani muhimu ya kuchangia kwa kuwa wao ndio wahusika wa taasisi hizo za utoaji wa taaluma ambazo zimegundulika kutokwenda sambamba na soko la ajira.
Amesema pamoja na kufanyiwa mapitio ya mara kwa mara mitaala ya taasisi hizo, utafiti unaonesha bado kuna pengo lililobainishwa hivyo kupitia rasimu hiyo ya Mafunzo na michango ya washiriki hao kunatajiwa kutoa muongozo thabiti wa kutatua na kuondosha kabisa tatizo hilo.
Pia Dkt. Ameir amebainisha kuwa kwa upande wa Zanzibar rasimu hiyo inakwenda sambamba na mpango wa Serikali wa Dira 2050 ambayo inasisitiza maendeleo ya rasilimali watu, ambayo inabainisha kwamba bila ya kuwa na ujuzi unaohitajika hatuwezi kuwa na watendaji ambao ni mahiri ambao watasaidia katika sekta mbalimbali kama vile afya, utalii, uchumi wa bluu na masuala mengine mbalimbali ya kimaendeleo.
Kwa upande wake Mshauri Elekezi Profesa Ntebe akiwasilisha rasimu hiyo kwa washiriki ameeleza kuwa, lengo zima la Mhe. Rais la kuleta Mpango wa Mafunzo Linganishi ni kuwasaidia wanafunzi wa VETA na wale wa Vyuo (Vikuu) waweze kupata nafasi za kufanya Mafunzo kwa Vitendo katika viwanda kwa kuwa viwanda ni sehemu ambayo wanaajirika.
Amesema kuwa tayari wameshaanza kuandika mpango huo kwa kushirikiana na timu iliyoundwa, na hivyo kufuatia maoni waliokusanya upande wa Tanzania bara, ndiyo sasa wamefika Zanzibar ili kuweza kukamilisha mpango huo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano WEMA.