
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu Khamis Abdullah Said, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Skuli binafsi ambazo zinatoa fursa Mbadala kwa watoto wa jamii ya kizanzibari na kutambua umuhimu wa skuli hizo kwa kuwaandaa vijana kuendana na mabadiliko ya dunia yanayoendelea kubadilika kwa kasi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wizara ya elimu Zanzibar Naibu katibu Mkuu Utawala Ndugu Amos John Henock wakati wa mahafali ya kwanza ya kidato cha nne ya Skuli ya Vivid Dream yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Nkrumah, Mfenesini Wilaya ya Magharibi A Unguja.
Ndugu Amos amewakumbusha wazazi na walezi kuwa jambo la msingi linalosaidia kwa kiasi kikubwa katika kutoa Elimu kwa watoto wetu ni kulipa ada kwa wakati kwani uendeshaji wa skuli hizo unahitaji rasilimali mbalimbali ili kutoa huduma bora na kufikia malengo wanayojipangia.
Aidha, naibu katibu mkuu amebainisha kuwa Wizara ya Elimu kwa sasa imepanua wigo na ufadhili wa Elimu ya Juu hadi kuwafikia wanafunzi wa Diploma hivyo ni jukumu la wanafunzi kusoma kwa bidii ili kuzipata fursa hizo.

Mapema bwana Henok amesema Taasisi ya Nur Alyaqeen Foundation inaunga mkono jihudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hususan katika masuala ya Huduma za Kijamii ikiwemo huduma za kielimu na afya.
Aidha ameushauri uongozi wa skuli binafsi kuweka ajira za kudumu zenye mikataba inayofahamika ambazo zitakuwa na mustakbali mwema kwa wafanyakazi ili kuwa na imani na amani muda wote wanapokuwa katika majukumu yao ya kazi zao za kila siku.
Akimkaribisha mgeni rasmi Afisa Elimu Mkoa wa Kaskazini Unguja Ndugu Subira Abdalla Vuai ameipongeza skuli ya VIVID kwa Kuandaa vyema kahafali yao ya kwanza kwa kidato cha nne na kuishukuru jumuiya ya skuli binafsi kwa kuendelea kutoa taaluma na kuipunguzia mrundikano wa wanafunzi katika skuli za Serikali.
Naye Mwakilishi wa Taasisi ya Nur Alyaqeen Foundation (NAYF) ambayo ndiyo mlezi wa Skuli ya Vivid Ndugu Makame Salim Ali akitoa historia ya Tasisi hiyo amesema kuwa Taasisi ya NAYF ilianzishwa mwaka 2016 na kusajiliwa rasmi mwaka 2017 baada ya wana jamii kuungana na kuona iko haja ya kuwa na Taasisi madhubuti itakayosimamia masuala mbalimbali kwenye jamii yetu yakiwemo masuala ya Kielimu chini ya kauli mbiu isemayo “NAYF for faith education and humanitarian services”. Ikiwa na malengo ya kuwaandaa vijana kuwa wazalendo wa nchi yao.
Alibainisha kuwa dunia ya leo inahitaji watu majasiri na wenye maono hivyo amewataka wahitimu na wanafunzi kwa ujumla kushikamana na mafunzo waliopatiwa wakiwa shuleni hapo ili kuibadilisha jamii kufikia ustawi ulio bora.
Imetolewa na Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano, WEMA.