
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema katika mwaka wa fedha ujao bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inatarajiwa kuongezeka kufikia trilioni moja.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar JUWASEZA uliofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Fidel Castro, amesema jitihada zinazofanywa na jumuiya hiyo zimepelekea ongezeko kubwa la kiwango cha ufaulu kwa Wanafunzi wa Zanzibar.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuthamini jitihada hizo kuongeza bajeti ya Wizara ya Elimu kutoka bilioni 864 hadi kufikia trilioni moja katika mwaka wa fedha ujao ili kuweza kuimarisha ubora wa Elimu nchini.
Aidha, Rais Mwinyi amewataka walimu wakuu kusimamia ipasavyo miundombinu ya elimu, ufaulu wa wanafunzi na rasilimali za umma, huku akiahidi kutenga fedha maalum kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu pale inapohitajika. Amewahakikishia walimu kuwa Serikali itaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Lela Mohamed Mussa, amesema mageuzi yanayoonekana katika sekta ya elimu yanatokana na maono na juhudi kubwa za Rais Mwinyi katika kusukuma maendeleo ya elimu Zanzibar.
Kabla ya kuzindua Mkutano wa JUWASEZA Mhe. Rais amezindua daghalia la wanawake Skuli ya Fidel Castro
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdallah Said, akiwasilisha taarifa ya kitaalamu, amesema ujenzi wa Dakhalia ya wasichana ya Skuli ya Fidel Castro umegharimu shilingi bilioni 1.5 na ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 288, kwa wastani wa wanafunzi 28 kwa kila darasa. Ameongeza kuwa wizara inatarajia kujenga Dakhalia nyingine 16 Unguja na Pemba katika mwaka wa fedha 2025–2026.