
Viongozi na watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuangalia vipaombele vya Wizara ya Elimu vilivyoainishwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2030, Dira ya Maendeleo ya 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati alipokutana na kutoa miongozo kwa viongozi wa ngazi mbali mbali kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwenye kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi.
Amesema Ilani ya CCM ya mwaka 2030 imeainisha mambo mahsusi ya kutekelezwa na Wizara ya Elimu pamoja na Hotuba ya Rais Dkt. Hussein Mwinyi aliyoitoa katika uzinduzi wa Baraza la 11 la Wawakilishi imefafanua vipaombele vya Serikali vya kutekelezwa na Sekta mbali mbali ikiwemo Sekta ya Elimu.
Mhe. Hemed amesema ili kufanikiwa kutekeleza mipango na mikakati ya Wizara iliyojipangia ni lazima viongozi wakasimamia suala la nidhamu na uwajibikaji kwa walimu na watumishi wengine ili kuweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza kuwepo kwa matumizi mazuri ya fedha na usimamizi wa mali za Serikali, sambamba na kuheshimu taratibu za ujazwaji wa mikataba ili kuweza kupata miradi yenye viwango bora.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewataka Wakurugenzi wa Wizara hiyo kufanya ufuatiliaji katika maeneo yao wanayoyaongoza ili kubaini changamoto mbali mbali zinazojitokeza na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.
Mhe. Hemed ameuagiza Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kusimamia haki, maslahi na stahiki za watumishi na kuharakisha uundwaji wa Tume ya Utumishi ya Walimu itakayosimamia maslahi na nidhamu za walimu.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Nane kwa kuendelea kuipa kipaombele sekta ya elimu kuanzia ngazi ya Maandalizi hadi Vyuo Vikuu.
Aidha, Waziri Lela amesema viongozi na watendaji wa Wizara ya elimu wapo tayari kuyafanyia kazi maagizo na maelekezo yote yanayotolewa na Serikali yenye lengo la kukuza na kuimarisha sekta ya Elimu nchini.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Tarehe: 03/12/2025.