
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mheshimiwa Lela Muhamed Mussa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Khadija Salum Ali wamefanya ziara ya kuzitembelea Taasisi ya Wizara hiyo zikiwemo Idara ya Michezo na Utamaduni na Baraza la Mitihani Zanzibar zilizopo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Lengo la ziara hiyo ni kuzikagua Taasisi, Vitengo na Idara ambazo zipo chini ya Wizara hiyo kwa lengo la kuzitambua na kujitambulisha kwa Watendaji hao, sambamba na kuelewa mafanikio na changamoto zilizopo katika Taasisi hizo ili ziweze kuongeza ufanisi katika Utendaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mhe. Lela amesema Wizara ya elimu ina jukumu kubwa la kuinyanyua Sekta ya Elimu na Utamaduni hivyo hakuna budi kwa watendaji hao kufanya kazi kwa jitihada kubwa ili kufikia maazimio ya Serikali ya kuona kwamba Elimu inaendelea kuwa kipaombele cha Taifa ili kujenga taifa liloimara na linaloendana na mabadiliko ya Teknolojia yanaoyokwenda sambamba na mabadiliko ya Dunia.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ndg. Khadija Salum Ali amewataka watendaji hao kuendeleza mashirikiano na kufuata sheria na miongozo iliyopo katika Idara zao pamoja na kufanya kazi kwa bidii, na Viongozi wa Wizara hiyo wako tayari kuwa karibu na kusikiliza changamoto zote na kuweza kuzitatua kwa mashirikiano ya pamoja hatua kwa hatua.
Nae Naibu Katibu Mkuu Utawala, Ndg. Amos John Henock ameahidi kufanya kazi kwa pamoja na Watendaji wote na wasisite kushirikiana na viongozi wakuu wa Wizara hiyo katika kila changamoto zinazowakabili ili ziweze kutatuliwa kwa muda sahihi.
Kwa upande wao watendaji wa Idara ya Michezo na Utamaduni pamoja na watendaji wa Baraza la mitihani wameushukuru Uongozi wa Wizara hiyo kwa kuweza kuwafikia na kuwasikiliza jambo ambalo limewapa fursa ya kutoa changamoto zao na wameahidi kuendeleza kufanya kazi kwa mashirikiano, bidii na kwa ufanisi mkubwa.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Uhusiano – WEMA.
Tarehe 02/12/2025.