THE Revolutionary Government of Zanzibar

Ministry of Education and Vocational Training

UFUNGAJI WA MAFUNZO YA TTT “ Training Teacher for Tomorrow”

Serikali imetowa wito kwa jamii hususan vijana kuweka uzalendo mbele katika matumizi ya teknolojia kwa maendeleo ya taifa letu na vizazi vinavyokuja. Wito huo umetolewa na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Mahamoud Thabit Kombo kwa njia ya mtandao wakati wa kufunga mafunzo ya siku kumi ya kuimarisha umahiri wa TEHAMA, hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu cha Nkrumah kiliopo Mfenesini, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Aidha Dkt. Kombo amesema; “Leo ni siku ya heshima kuu kwangu kushiriki nanyi katika kufunga rasmi programu muhimu ya maendeleo ya kitaaluma katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu. Tangu tarehe 10 hadi 21 Novemba 2025, walimu 35 wa sekondari na maafisa wa TEHAMA wamepata mafunzo makubwa na ya kubadilisha mtazamo, wakiboresha ujuzi wao na uwezo wa kulitumikia taifa letu.

Ninatoa shukrani za dhati kwa washirika wetu wote waliowezesha kufanyika kwa programu hii. Tulianza safari hii nilipokuwa Balozi, na leo tumefika hatua ya kuona matunda yake kwa macho yetu wenyewe, asanteni sana kwa dhamira yenu isiyotetereka.

Ushirikiano wenu unaonyesha kwa uwazi dhamira ya kuwawezesha vijana wetu, kupanua fursa, na kuhakikisha kuwa mapinduzi ya kidijitali yanawafikia wananchi katika kila kona ya Tanzania. Kwa washirika wetu wa Italia na Mheshimiwa Balozi aliyeungana nasi leo mtandaoni, jambo hili linaonyesha namna uhusiano wa kimataifa unavyojenga uwezo wa rasilimali watu barani Afrika na nchini kwetu. Tunatambua na kuthamini kwa dhati mchango wenu.

Kile mnachokifanya ni uwekezaji katika watu wetu—walimu wetu ambao ni mhimili wa uchumi wa maarifa; maafisa wetu wa TEHAMA ambao ni injini ya kisasa ya mifumo ya serikali; na hatimaye vijana wetu ambao watanufaika kupitia mbinu mpya na ufundishaji bora utakaopelekwa shuleni.
Niruhusuni niseme wazi kuwa teknolojia tunayoipata leo ni lazima itumike kwa manufaa ya nchi na kwa uzalendo. Tumeshuhudia katika siku za karibuni jinsi nguvu ya mitandao ya kijamii ilivyotumiwa kushambulia nchi yetu kutoka nje. Baadhi ya watu wenye ujuzi mkubwa wa TEHAMA wanaweza kutumia teknolojia vibaya na bila uzalendo, jambo ambalo ni hatari na halikubaliki.

Hivi karibuni, tulilazimika kuzima mtandao wa intaneti na mifumo ya TEHAMA kwa muda mfupi kutokana na mashambulizi ya kimtandao yaliyolenga kuleta taharuki nchini. Sote tulishuhudia hilo, hata Mheshimiwa Balozi akiwa ofisini kwake.
Hivyo basi, ninawaomba tuweke uzalendo mbele katika matumizi ya teknolojia kwa maendeleo ya Taifa letu na vizazi vinavyokuja.Asanteni sana kwa kunisikiliza, kwa ushirikiano wenu, na kwa kujitoa kwenu katika kuijenga Tanzania mpya yenye uwezo wa kukabiliana na dunia ya kidijitali”.

Awali akimkaribisha Waziri huyo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndg. Khamis Abdulla Said ametoa shukrani maalum kwa wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa TEHAMA na timu nzima ya wizara, pamoja na timu ya ROSA, ambao wamethibitisha kujitoa kwao bila kuyumba. Ameongeza kuwa ushirikiano, muda na utaalamu wao umeimarisha uwezo wa watumishi wetu na taasisi zetu.

Ndg. Said amefahamisha kuwa, kuhitimisha programu hii muhimu ya maendeleo ya kitaaluma kunalenga kuimarisha umahiri wa TEHAMA na ujuzi wa elimu ya kidijitali katika sekta yetu ya elimu, na kutoa shukrani za dhati kwa washiriki wote walimu, maafisa wa TEHAMA, wataalamu wetu wa ndani, na wadau mbalimbali kwa mchango wao wa thamani katika kufanikisha mafunzo haya.

Nae Balozi wa Italy nchini Tanzania bwana Joe Coppola amesema kuanzishwa kwa mafunzo kutaimarisha mashiriano yaliyopo baina ya Italy na Zanzibar, na kubainisha kua mafunzo hayo ni muhimu kwani teknolojia ya mawasiliano ni muhimu kwa maisha ya sasa.

Mafunzo hayo ya siku 10 yaliyojulikana kwa jina la “ Training Teacher for Tomorrow” yametolewa na Taasisi isiyo ya Kiserikali (NGO) ya ROSA ya Italia ikiongozwa na Bi Maria na timu yake.

Imetolewa na Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano – WEMA.