
Naibu Katibu Mkuu Utawala wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (WEMA), Nd. Khalid Masoud Wazir, leo tarehe 19/11/2025 ameongoza kikao cha pamoja cha majadiliano baina ya Taasisi ya Teknolojia ya India Madras Kampasi ya Zanzibar (IITMZ) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST) kilichojadili mpango wa ufadhili wa wanafunzi watakaodahiliwa kuingia katika Taasisi ya IITMZ kupitia Samia Scholars.
Majadiliano hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizi mbili, kubainisha maeneo ya utekelezaji wa programu ya ufadhili, pamoja na kuhakikisha kuwa wanufaika wa Samia Scholars wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kufanikiwa katika taaluma za sayansi na teknolojia zinazotolewa na IITMZ.

Maeneo mengine ya majadiliano yamegusia uratibu wa pamoja kati ya wizara hizo mbili na IITMZ, vigezo vya uteuzi wa wanufaika, pamoja na kuhakikisha mifumo ya udahili, usimamizi wa ufadhili na ufuatiliaji wa maendeleo ya wanafunzi inakwenda sambamba na malengo ya mpango wa Samia Scholars.
Katika kikao hicho ujumbe wa IITMZ umeongozwa na Mkurugenzi Dhamama wa Taasisi hiyo Pro. Preeti Aghalayam, Pro. K. Suresh Msimamizi Mkuu Taaluma na kwa upande wa MoEST ujumbe uliongozwa na Pro. Makenya Maboko ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Programu (Scholarship Program Committee) ya Samia Scholarship Extended (SSE) DS/AI+, Dk. Maryam Ismail Kaimu Mkurugenzi Idara ya Elimu ya Juu (DHE).
Wajumbe wengine ni kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Kitaaluma (NACTVET).
Imetolewa na Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar