Walimu wametakiwa kuifanyia kazi taaluma wanayopewa katika mafunzo ili kuwajengea weledi wanafunzi na kuinua sekta ya elimu kivitendo.
Hayo yameelezwa leo 12/09/2025 na Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo ya Ualimu Ndg Othman Omar Othman wakati akifungua warsha ya mafunzo kwa walimu wa Hisabati, Kiingereza na Sayansi katika Kituo cha Walimu Bububu, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Mafunzo hayo ya siku 15 yana lengo la kukuza kiwango cha ufanisi kwa wanafunzi jambo ambalo haliwezi kufikiwa bila ya kuwapatia walimu mafunzo bora na kuimarisha viwango vyao kitaaluma kwani bila ya shaka kuafaulu kwa mwalimu ndiyo hupelekea ufaulu mzuri kwa mwanafunzi na kinyume chake.
Aidha ndg Othman amesisitiza kuwa kutakuwa na upimaji kabla na baada ya mafunzo hayo ili kupata tathmini juu ya kiwango cha ufanisi kitakwimu ili kuweka data halisi kwa walimu waliopatiwa mafunzo na matokeo ya mafunzo hayo kwa lengo la kukuza kiwango cha ufanisi kwa ngazi zote za kielimu.
Kwa upande wake Mratibu wa Kituo hicho cha Ualimu Mwalimu Daudi Mohamed Ali amewataka walimu hao kutumia busara zao kuwaasa wanafunzi kujiepusha na kujiingiza katika mambo yasiyowahusu kama vile kufuata ngoma wakiwa skuli au njiani wanapokwenda au kurudi skuli hasa katika kipindi hiki kuelekea harakati za uchaguzi nchini.
Imetolewa na Kitengo cha Habari, Elimu na Uhusiano, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA), Zanzibar.