
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mh. Ali Abdulghulam Hussein, amesema uzinduzi wa mradi wa afya ya akili katika skuli za Zanzibar, kutaimarisha mazingira ya maendeleo ya elimu kwa walimu na wanafunzi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huko mbweni amesema afya bora ya akili huongeza uelewa, ubunifu na maamuzi sahihi kwa walimu na wanafunzi, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha mazingira ya elimu yanakuwa salama.
Amesema azma ya Serikali ya kujenga uchumi imara itafikiwa endapo kutakuwa na wanafunzi wenye uwezo mkubwa kitaaluma na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Naye mratibu wa shirika la kusaidia elimu ya afya ya akili Zanzibar Lady’s Fatemah Trust, Mukhtar Karim, amesema tayari walimu na wakufunzi wameshapatiwa elimu ya afya ya akili ili kuifikisha kwa walimu wengine.
Kwa upande wake, daktari wa afya ya akili kutoka hospitali ya kivunge, Maryam Haji Mussa na Khalfan Abdallah Nassour kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar, wamesema kupitia mradi wa akili timamu, akili bora, utastawisha maendeleo ya upatikanaji wa elimu na kuongeza uelewa kwa walimu.
Imetolewa na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano (WEMA).