Mnamo tarehe 4 Agosti 2025, Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar ilipokea ugeni maalum kutoka Ujerumani, ukiongozwa na Bw. Thilo Turke, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa taasisi ya YESSS, pamoja na Bi. Martina Coeffier, mshauri mwelekezi katika masuala ya ushonaji na urembo.
Ugeni huo ulitembelea Ofisi Kuu ya Mamlaka hiyo na kupokelewa rasmi na Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Bakari Ali Silima. Pia walitembelea Chuo cha Amali Mkokotoni kilichopo Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Lengo kuu la ziara hiyo lilikuwa kujadili na kuangazia maeneo ya ushirikiano katika sekta ya mafunzo ya amali, hususan kuanzishwa kwa mfumo wa utoaji wa mafunzo kwa njia ya Dual Apprenticeship — mfumo unaojumuisha mafunzo ya vitendo kazini na ya nadharia darasani, kwa ushirikiano na taasisi binafsi.
Kupitia kikao hicho, pande zote mbili zimeonesha nia ya dhati ya kushirikiana katika kukuza ujuzi na stadi za kazi kwa vijana wa Zanzibar, hasa katika fani ya ujenzi, kwa lengo la kuwawezesha kujitegemea kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika soko la ajira la ndani na kimataifa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar
Tarehe: 6 Agosti 2025