Zanzibar, 04 Agosti 2025 – Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Mambo ya Utalii na Mambo ya Kale, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar (VTA), na TUI Care Foundation, imesaini Hati ya Ushirikiano (MoU) yenye lengo la kukuza na kuendeleza sekta ya urithi na utalii wa kihistoria visiwani Zanzibar.
Makubaliano hayo yanalenga kuanzisha mfumo wa masomo ya utalii kupitia mtandao (e-learning), yatakayowasaidia vijana wa Zanzibar kupata ujuzi unaohitajika katika soko la kimataifa la ajira kwenye sekta ya utalii.
Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika katika Ukumbi wa Idrissa Abdul Wakil, Kikwajuni – Unguja, na kushuhudiwa na wadau wakuu kutoka pande zote tatu, wakiwemo:
Dkt. Bakari Ali Silima, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar,
Bw. Alexander Panczuk, Mkurugenzi Mkuu wa TUI Care Foundation,
Dkt. Aboud Suleiman, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Kale.
Kupitia mkataba huo utaweza kuwajengeaa vijana uwezo na ujuzi wa kushiriki kikamilifu katika sekta ya utalii kupitia mitaala ya mafunzo ya kazi (career tourism curriculum).
Kuanzisha mfumo wa mafunzo ya kimtandao (professional online program) utakaowawezesha zaidi ya vijana 200,000 kupata mafunzo na kuhitimu kwa vyeti vinavyotambuliwa na TUI Care Foundation.
Kuweka misingi ya utoaji wa mafunzo ya moja kwa moja (live training platform) na huduma za kitalii kupitia vituo maalum vya mafunzo vitakavyosimamiwa na VTA.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Bakari Silima alitoa shukrani kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Wizara ya Mambo ya Kale kwa mchango wao mkubwa, amesema Mamlaka yetu itahakikisha inajenga uelewa kwa jamii juu ya umuhimu wa utalii wa kimataifa kupitia ushirikiano huu na TUI Care Foundation.
Kwa upande wake, Dkt. Mwanahamis Adam Ameir, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, alieleza kuwa serikali imeanza mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kuingiza mtaala wa Amali kwenye ngazi ya sekondari, ambapo masomo ya utalii yatakuwa sehemu muhimu. Mafunzo haya yatafundishwa kwa Kiswahili na Kiingereza ili kuhakikisha ushirikishwaji mpana wa vijana.
Naye Dkt. Aboud Suleiman kutoka Wizara ya Mambo ya Kale, aliipongeza TUI Care Foundation kwa mchango wake mkubwa na kueleza kuwa kuna mikakati ya kuvutia taasisi za ndani na nje ya nchi kushiriki katika kuendeleza sekta ya utalii wa urithi visiwani Zanzibar.
Chuo cha TUI Foundation kinatarajiwa kutoa mafunzo bure, ikiwa ni hatua ya kusaidia vijana wa Zanzibar kuelewa namna ya kujihusisha na masoko ya utalii kimataifa.
Mkataba huu wa ushirikiano unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa jamii ya Zanzibar, kwa kuongeza fursa za ajira, kukuza maarifa na ujuzi wa vijana, na kuchangia maendeleo endelevu ya sekta ya utalii wa urithi visiwani.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar
04 Agosti 2025