
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Lela Muhamed Mussa ambae pia ni Makamu wa Rais wa Chama cha Skauti Tanzania leo tarehe 19/07/2025 amekutana na Viongozi na Skauti wote wa Unguja katika Ukumbi wa Dkt. Mohamed Shein Tunguu, Mkoa wa Kusini – Unguja.
Lengo la kikao hicho ni kuendeleza umoja, mshikamano, kujuana, uzalendo na uwajibikaji katika majukumu yao ya kila siku na kujenga taifa imara kwa maslahi ya Tanzania.
Waziri Lela amesema, amefurahishwa na Vijana wa Chama hicho ambao wameonesha kwa vitendo namna walivyowiva katika maadili, uzalendo na kujielewa jambo linaloleta faraja kwa kuwajenga wanafunzi hao kua Viongozi na raia wema kwa taifa.
Akitoa pongezi kwa walimu wa wanafunzi hao
Mheshimiwa Lela amesema mafunzo hayo ya ziada ambayo wanapatiwa wanafunzi hao kupitia chama cha Skauti yanaenda sambamba na matakwa ya Mtaala wa Elimu ya Zanzibar kwa kuwapa wanafunzi elimu ya ziada inayowajengea Ukomavu na akakamavu kuanzia ngazi ya chini na kutoa wito kwa wazazi na walezinkuendelea kuwashajihisha watoto wao kujiunga na Chama hicho na Serikali itaendelea kuwasimamia vyema na inafurqhishwa sana na kazi nzuri zinazoendelea kufanywa na Vijana wa Skauti.
Mheshimiwa Lela ameahidi kuzitatua Changamoto zote hatua kwa hatua na kuendelea kutoa mashirikiano na waendelea kuiamini na kushirikiana na Wizara ya Elimu wakati wote.
Nae mjumbe wa Bodi ya Skauti kwa upande wa Zanzibar Inspekta Mtumwa Khamis amesema wataendelea kukilea Chama cha Skauti kwa Zanzibar ili kiende sambamba na matakwa ya Skauti kwa Dunia kwa ujumla.
Akisoma Risala kwa niaba ya Skauti Kamishna Mkuu Msaidizi Mazingira na Makambi wa Chama cha Skauti Tanzania Ndg. Mwanaidi Silima Khamis ameushukuru Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa kuendelea kukipa mashirikiano Chama hicho jambo ambalo linawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.
Akieleza changamoto zinazowakabili amesema kwa sasa uhaba wa bajeti ninkikwazo kinachopelekea kutofikia baadhi ya malengo waliojiwekea, hivyo ameiomba Serikali kuwawezesha Skauti hao katika shuhuli za ujasiriamali ili iwasaidie kujiendesha wenyewe
Imetolewa na Kitengo Cha Habari, Elimu na Uhusiano Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.