
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kupitia Idara ya Michezo na Utamaduni imesema, itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wanafunzi wanamichezo kwa lengo la kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vyao vya michezo.
Ameyasema hayo Mkurugenzi Idara ya Michezo na Utamaduni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bi. Hafsa Aboud Talib wakati akizungumza katika hafla ya chakula cha pamoja na wanafunzi wa michezo katika ukumbi wa Kituo cha Walimu (TC) cha Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B”, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Amesema lengo la hafla hiyo ni kufuatia ahadi ya Idara hiyo kwa Wanamichezo hao kutokana na ushindi mkubwa walioupata katika mashindano ya UMISSETA yaliyofanyika Mkoani Iringa Tanzania Bara.
Aidha, Bi. Hafsa ameendelea kuwapongeza vijana hao na kuwataka kuendeleza bidii katika masomo yao lakini pia katika michezo ili waweze kuwa vijana bora.
Amesema, Michezo hujenga afya na pia vijana wataweza kujiajiri na kuajirika katika nyanja mbalimbali Kitaifa na Kimataifa. Hivyo ni vyema kujiwekea mustakbali mwema wa maisha yao.
Nae Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Michezo wa Idara hiyo Ndg. Tahir Mkubwa Said amewasisitiza vijana hao kuzidisha bidii na kuendelea na mazoezi ya michezo mbali mbali inayoratibiwa na Idara hiyo kwa lengo la kuiletea Zanzibar ushindi zaidi na kuitangaza Zanzibar ndani na nje nchi.
Akitoa shukurani kwa niaba ya wanamichezo wenzake Ndg. Bilali Abdalla Hassan kwa Uongozi wa Idara hiyo kwa mashirikiano makubwa waliyowaonesha na kuwapa moyo pamoja na kuwajali katika kukuza na kuendeleza vipaji vyao.
Amesema awali jambo hilo halikuwepo na hivyo kuiomba Idara kuendeleza utaratibu huo kwa awamu zijazo ili lengo liweze kufikiwa. Pongezi hizo pia watapatiwa wanafunzi wanamichezo walioshiriki UMISSETA kwa upande wa Pemba
Imetolewa na kitengo cha Habari, Elimu na uhusiano, Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali (WEMA) Zanzibar.