
Naibu Katibu Mkuu Utawala Wizara ya Elimu na Mafunzo Zanzibar Ndugu Khalid Masoud Waziri leo tarehe 15/07/2025 ameiongoza timu ya wataalamu ya Wiara hiyo katika mkutano uliowahusisha wawakilishi wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) uliofika ofisini hapo Mazizini Mjini Unguja.
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mpango wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu Zanzibar kufuatia Wizara hiyo kurejesha mafunzo ya Ualimu ambayo awali yalitolewa kapitia Chuo cha Nkrumah ambacho kwa sasa kimesitisha utoaji wa taaluma hiyo.
Naibu khalid amebainisha kuwa Wizara inatarajia kutiliana saini hati ya makubaliano (MoU) mapema mwaka 2026, hivyo ameitaka timu hiyo ya wataalamu kukaa kwa pamoja na kujadili kwa kina maeneo muhimu katika ujenzi wa Chuo hicho kwa lengo la kuleta tija na ufanisi kwa maslahi mapana ya taifa letu.
Kwa upande wao Bw. Shin na Bw. Han kutoka KOICA wamesema ujenzi wa chuo hicho unatarajiwa kuanza ifikapo mwaka 2028 ambapo aliwasilisha michoro mbalimbali ya mwonekano wa majengo ya chuo hicho na kuwataka wadau hao kutoa maoni ya kuboresha na kufanikisha shughuli hiyo.
Timu ya wataalamu iliwahusisha Wahandisi wa Wizara ya Elimu, Wajumbe kutoka Idara ya Mafunzo ya Ualimu, Taasisi ya Elimu ya Zanzibar na baadhi ya maafisa wa Wizara hiyo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari, Elimu na Uhusiano,
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (WEMA).