
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhamed Mussa, leo amekabidhi vyeti kwa wahitimu wa Shahada ya Pili kutoka Taasisi ya Teknolojia ya India Madras (IIT Madras), Kampasi ya Zanzibar.
Mahafali hayo ya kihistoria yamefanyika katika viunga vya kampasi ya IITMZ, yakiwa ni mahafali ya kwanza tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwezi Oktoba 2023.
Jumla ya wanafunzi 16 wamehitimu masomo yao kwa mwaka wa masomo 2023–2025. Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Elimu, taasisi za elimu ya juu, pamoja na wadau wa elimu kutoka ndani na nje ya nchi.
Waziri Lela amewapongeza wahitimu kwa juhudi na uvumilivu wao katika kufanikisha masomo yao, na kuipongeza IIT Madras kwa mchango wake mkubwa katika kuinua kiwango cha elimu ya juu Zanzibar kupitia ushirikiano wa kimataifa.
Kampasi ya IITMZ ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya India, na inalenga kutoa elimu ya kiwango cha juu katika teknolojia na ubunifu kwa vijana wa Zanzibar na kimataifa kwa ujumla.
Imeyarishwa na
Kitengo cha Habari naUhusiano
Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali
Zanzibar .