Zanzibar, 17 Juni 2025 – Walimu 102 kutoka skuli 34 zinazohudumiwa na Kituo cha Walimu Kiembesamaki wamehitimu rasmi mafunzo ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ufundishaji na ujifunzaji, katika mahafali yaliyofanyika leo.
Mafunzo hayo ya muda wa miezi mitatu yameendeshwa na Idara ya TEHAMA katika Elimu kwa ushirikiano na Kituo cha Walimu Kiembesamaki, yakilenga kuwawezesha walimu kutumia teknolojia kisasa katika kuimarisha mbinu za ufundishaji darasani. Washiriki wa mafunzo hayo walikuwa ni pamoja na Walimu wa Sayansi na Teknolojia, Walimu Wataaluma pamoja na walimu kutoka masomo mbalimbali ya sekondari na msingi.
Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu – Taaluma, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Maandalizi na Msingi, Ndugu Ali Mussa, aliwataka walimu hao kuhakikisha wanatumia ujuzi walioupata katika kuinua kiwango cha elimu kupitia matumizi bora ya TEHAMA. Alisisitiza kuwa kwa dunia ya leo inayobadilika kwa kasi kiteknolojia, hakuna nafasi tena ya kufundisha kwa mbinu za kizamani, na hivyo walimu wanapaswa kwenda sambamba na mabadiliko hayo
Kwa upande wao, baadhi ya walimu waliohitimu walieleza kufurahishwa kwao na mafunzo hayo, wakisema yamewajengea uwezo mkubwa wa kutumia kompyuta, programu za kielimu, mitandao ya kijamii kwa elimu, na mbinu shirikishi za kidigitali darasani.
Mahafali hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA kwenye sekta ya elimu, kwa lengo la kuwaandaa wanafunzi kuwa washindani katika soko la ajira linalozidi kuathiriwa na maendeleo ya teknolojia duniani.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali – Zanzibar
Tarehe: 17 Juni 2025.